Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano
na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo
Aprili 17, 2026.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) Mhe. Ridhiwani Kikwete bungeni jijini Dodoma leo Aprili 17, 2026. Kulia ni Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Kundo Mathew.******************
Serikali imesema itaendelea kuimarisha juhudi
za kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha na kushiriki kikamilifu
katika biashara ya kaboni ili kunufaika kiuchumi huku wakichangia uhifadhi wa
mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano
na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge
wa Viti Maalumu Mhe. Josephine Kapoma aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani
wa kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu biashara ya kaboni.
Akijibu swali hilo bungeni jijini Dodoma leo
Aprili 17, 2026, Mhe. Kwagilwa alisema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais
na Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) zimeweka mikakati mbalimbali ya
kufikisha elimu kwa wananchi.
Alitaja mikakati hiyo kuwa ni kuongeza uelewa
wa wananchi kuhusu dhana, faida na fursa zilizopo katika biashara hiyo kupitia
vyombo vya habari na kutoa mafunzo kwa viongozi wa ngazi za mikoa, halmashauri
na vijiji ili waweze kuwa mabalozi wa elimu kwa jamii zao kuhusu utekelezaji wa
miradi ya kaboni na manufaa yake.
“Tangu kupitishwa kwa Kanuni na Mwongozo wa
Biashara ya Kaboni tumetoa elimu kwa viongozi mbalimbali pamoja na kushirikiana
na wadau wa maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi katika kutoa elimu na
kujenga uwezo kwa jamii kuhusu namna ya kuanzisha na kunufaika na miradi ya
kaboni,” alisema Mhe. Kwagilwa.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kwagilwa
alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar zinashirikiana katika kutekeleza miradi ya mazingira na
kunufaisha wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza
la Mbunge wa Jimbo la Amani Mhe. Abdul Yussuf Maalim aliyetaka kufahamu
Zanzibar inanufaika vipi na biashara ya kaboni.
Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Kwagilwa
alisema pamoja na kushirikiana katika biashara ya kaboni pia Serikali zote
mbili zinashirikiana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi.
Ikumbukwe kuwa biashara ya kaboni ni mfumo wa
kifedha unaoruhusu nchi, taasisi au miradi kupunguza uzalishaji wa gesi joto na
kupata faida kwa kuuza au kubadilishana hati za kaboni ambazo hutolewa unapofanikiwa
kupunguza au kufyonza hewa ya kaboni.
No comments:
Post a Comment