Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo akiambatana na afisa elimu na mawasiliano TRA mkoa wa Kagera Bw. Ruekaza Rwegoshora wametoa elimu juu ya madhara ya magendo kupitia redio KDCU Fm iliyoko Kayanga Karagwe mkoani Kagera.
Elimu hiyo imetolewa leo tarehe 16 Machi, 2026 kwa wananchi ambapo Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano Bw. Kayombo amesema biashara za magendo zina athari kubwa kwa jamamii na taifa kwa ujumla hivyo kila mwananchi anatakiwa kuwa mzalendo na kukataa magendo kwa nguvu zote.
Bw. Kayombo amesema magendo yanaweza kuhatarisha afya, usalama, kuleta ushindani usio sawa na kuikosesha serikali mapato hivyo kuchelewesha maendeleo ya Taifa.
“Biashara za magendo zina athari kubwa kwani zinaweza kuhatarisha afya, usalama, kuleta ushindani usio sawa na kuikosesha serikali mapato” amesema Bw. Kayombo.
Kwa upande wake afisa elimu na mawasilliano wa TRA mkoa wa Kagera Bw. Ruekaza Rwegoshora amesema mtu yeyote akikamtwa na magendo atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo; kutaifisha chombo cha moto kilichotumika kubeba magendo, kupigwa faini, kifungo au vyote kwa pamoja hivyo kuwahimiza wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kutumia njia rasmi na kufuata taratibu zote za kiforodha kuingiza na kuondosha bidhaa nje ya nchi.
Aidha wananchi wameombwa kutoa taarifa kupitia simu namba 0784 210 209 endapo wataona bidhaa zinapitishwa kwa njia ya magendo au vitendo vya ukwepaji kodi na zawadi ya asilimia 3 ya kodi itakayokusanywa hapo itatolewa kwa atakayetoa taarifa.

No comments:
Post a Comment