Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa Italia nchini Tanzania Mheshimiwa Giuseppe Sean Coppola, na ujumbe kutoka DANIELI Group, Ikulu, Dar es Salaam tarehe 29 Machi, 2026..jpeg)
.jpeg)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amefanya mazungumzo na
Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mheshimiwa Giuseppe Sean Coppola,
aliyemtembelea Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Balozi huyo aliambatana na
ujumbe kutoka Danieli Group, kampuni inayoongoza duniani katika teknolojia na
uhandisi wa uzalishaji wa chuma, ambao wameonesha nia ya kuchunguza uwezekano wa kuwekeza katika sekta
ya chuma nchini Tanzania.
Katika mazungumzo hayo, ujumbe
huo uliwasilisha nia ya kuanzisha mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kisasa na
kikubwa cha chuma mkoani Mtwara, kwa kushirikiana na mwekezaji mzawa.
Ushirikiano huu unatokana na
majadiliano ya awali yaliyofanyika wakati wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji
kati ya Tanzania na Italia, pamoja na mashauriano ya kitaalamu yaliyofuata na
taasisi za Tanzania, ikiwemo Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji Tanzania
(TISEZA) na wizara husika.
Mradi unaopendekezwa, ambao
bado uko katika hatua ya awali ya uchambuzi, unakadiriwa kugharimu takribani
Euro bilioni 1.5 (sawa na takribani Shilingi trilioni 4.2 za Kitanzania), na
unatarajiwa kutekelezwa kwa awamu kulingana na tathmini zaidi na taratibu za
uwekezaji.
Akizungumza katika kikao
hicho, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alikaribisha nia hiyo na kusisitiza
dhamira ya Tanzania kuendeleza uwekezaji wa kimkakati unaoendana na vipaumbele
vya taifa.
“Tanzania inaendelea kujijenga
kama kituo shindani na cha kuaminika kwa uwekezaji, ikitegemea rasilimali zake
asilia, nafasi yake ya kimkakati, pamoja na mageuzi yanayoendelea kuboresha
mazingira ya biashara,” alisema.
Aliongeza kuwa, “Tunakaribisha
ushirikiano unaoongeza thamani ya rasilimali zetu, unaozalisha ajira kwa
wananchi wetu, na kuchangia dira yetu ya muda mrefu ya kujenga uchumi wa
viwanda.”
Kwa upande wake, Balozi wa
Italia alieleza kuwa ushirikiano huo unaakisi kuimarika kwa mahusiano ya
kiuchumi kati ya Tanzania na Italia chini ya mifumo mipana ya ushirikiano wa
maendeleo.
“Nia iliyooneshwa na Danieli
Group ni sehemu ya juhudi pana za kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zetu
mbili, ikiwemo kupitia Mpango wa Mattei kwa Afrika,” alisema.
Aliongeza kuwa, “Mpango huu
unalenga kukuza uwekezaji endelevu na wenye manufaa kwa pande zote, na Tanzania
inaonekana kuwa mshirika muhimu katika muktadha huu.
Kwa sasa, tupo katika hatua ya
kuangalia uwezekano na tunatarajia kuendelea kushirikiana kwa karibu na
Serikali ya Tanzania kadri majadiliano yatakavyoendelea.”
Naye Mtendaji Mkuu wa Danieli
Group, Bw. Giacomo Mareschi Danieli, alieleza sababu za kimkakati zilizoifanya
kampuni hiyo kuvutiwa na Tanzania.
“Tunaona fursa kubwa nchini
Tanzania, si tu kutokana na uwepo wa rasilimali kama gesi na madini ya chuma,
bali pia kutokana na ukuaji wa soko na nafasi yake ya kimkakati katika ukanda
huu,” alisema.
“Mtazamo wetu unalenga
ushirikiano wa muda mrefu - kuleta teknolojia ya kisasa inayozingatia
mazingira, huku tukishirikiana na wadau wa ndani kukuza ujuzi na kujenga uwezo
endelevu wa viwanda. Hii ni hatua ya awali, na tumejipanga kuendelea na majadiliano
ya kitaalamu ili kutathmini uwezekano wa mradi huu,” aliongeza.
Iwapo utatekelezwa, uwekezaji
huu unaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ajenda ya Tanzania ya kujenga
uchumi wa viwanda chini ya Dira ya Taifa ya 2050, kwa kuimarisha uzalishaji wa
ndani wa chuma, kupunguza uagizaji kutoka nje, kuongeza thamani ya rasilimali
za ndani, na kutengeneza ajira kwa vijana.
Aidha, unaweza kuimarisha
nafasi ya Tanzania kama kitovu cha uzalishaji wa chuma katika ukanda huu,
hususan kwa nchi jirani zisizo na bandari, pamoja na kusaidia maendeleo ya
miundombinu na usafirishaji katika ukanda wa Mtwara.
Mheshimiwa Rais Samia
alimhakikishia Mheshimiwa Balozi na ujumbe wake kuwa Serikali itaendelea kuwa
wazi kwa wawekezaji wenye sifa, wanaoleta si mtaji pekee bali pia teknolojia,
ujuzi na dhamira ya muda mrefu katika maendeleo ya Tanzania.
Kikao hicho kimeonesha
kuendelea kuimarika kwa mvuto wa Tanzania kama kituo cha uwekezaji, pamoja na
dhamira ya pamoja ya pande zote mbili kuendelea kuchunguza fursa zitakazozalisha
thamani endelevu ya kiuchumi na ukuaji shirikishi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Balozi wa Italia nchini Tanzania Mheshimiwa Giuseppe Sean Coppola pamoja na ujumbe kutoka DANIELI Group, Ikulu, Dar es Salaam tarehe 29 Machi, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Mkurugenzi na Mmiliki wa DANIELI Group Bw. Giacomo Mareschi-Danieli, Ikulu, Dar es Salaam tarehe 29 Machi, 2026.




No comments:
Post a Comment