January 28, 2026

SERIKALI YATOA MIKOPO KIASI CHA SHILINGI MILIONI 600 KWA WANANCHI





Halmashauri ya Mji Ifakara Januari 27,2026 imetoa mikopo ya asilimia 10 yenye thamani ya Shilingi milioni 600 ikiwa ni Mikopo ya Asilimia 10 inayotokana na Mapato ya ndani  kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ikiwa ni utekelezaji wa sera ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo hiyo iliyofanyika katika Viwanja vya Stendi ya mabasi kibaoni  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felista Mdemu, ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba.

Mdemu amevitaka vikundi vilivyonufaika kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa, kuzingatia masharti ya mikataba, pamoja na kurejesha mikopo kwa wakati ili kutoa fursa kwa wananchi wengine kunufaika.

 Shilingi 404,787,300 tayari imekwishatolewa kwa vikundi 41, vikiwemo vikundi 20 vya wanawake, 17 vya vijana na 4 vya watu wenye ulemavu na  Shilingi 195,212,700 zitatolewa kwa vikundi 17 vilivyosalia mara baada ya kukamilisha maboresho yaliyoelekezwa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara, Pilly Kitwana amewasihi wananchi wa Halmashauri ya Mji Ifakara kuendelea kuunda Vikundi kwani pesa bado zipo ambazo zitasaidia kuwainua pia ameahidi kuendelea kufanya tathimini na  ufuatiliaji kwa vikundi vilivyonufaika ili kuhakikisha mikopo hiyo inaleta tija na kuchangia maendeleo ya kiuchumi kwa wanufaika na jamii kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment