January 31, 2026

DIAMOND AIPONGEZA JAB, AAHIDI VYOMBO VYAKE KUTII SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI

Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi wa Wasafi Media, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz, ameipongeza Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, huku akiahidi kuwa vyombo vyake vya habari viko tayari kufuata kikamilifu matakwa yote ya kisheria yanayoongoza sekta ya habari nchini.

Diamond ametoa kauli hiyo baada ya kufika katika ofisi za Bodi ya Ithibati kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari, akisema Wasafi Media haina nia ya kukwepa sheria bali ina dhamira ya kushirikiana kwa karibu na wasimamizi wa taaluma ya uandishi wa habari.

Amesema licha ya Sheria hiyo kuleta changamoto kwa baadhi ya vyombo vya habari na watumishi wake, bado haiwezi kupingwa kwani ilitoa muda wa kutosha kwa wadau wote kujipanga na kutimiza vigezo vilivyowekwa, ikiwemo sharti la waandishi wa habari kuwa na kiwango cha elimu cha kuanzia Diploma na kuendelea.
Diamond amekiri kuwa kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari kumeleta nidhamu na uwajibikaji mkubwa katika taaluma ya habari, akisisitiza kuwa Wasafi Media inaunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha weledi, maadili na heshima ya taaluma hiyo inalindwa.

“Sisi hatutaki kukwepa utekelezaji wa Sheria. Hakuna namna unaweza kuvunja Sheria na ukabaki salama. Tumehakikisha watumishi wetu wote wanazingatia Sheria na katika hilo sina utani,” amesema Diamond.

Aidha, amesema hapo awali alipata taarifa na tafsiri tofauti kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, hali iliyosababisha sintofahamu kwa baadhi ya wadau, lakini baada ya kufika katika ofisi za Bodi na kupewa ufafanuzi wa kina, ameelewa vyema dhamira ya Serikali ya kuimarisha taaluma ya habari nchini.

Amepongeza pia msimamo wa Waziri mwenye dhamana aliyesisitiza kuwa Bodi ya Ithibati ni mlezi wa waandishi wa habari, akisema baada ya mazungumzo na uongozi wa Bodi, ameridhishwa kuwa taasisi hiyo ipo kwa ajili ya kulinda na kukuza taaluma hiyo, si kuibana.
“Nakiri wazi kuwa Bodi ni mlezi kwa waandishi wa habari. Baada ya kuielewa Sheria vizuri, hakuna sababu ya kupingana nayo. Watu wangu tayari wamechukua hatua stahiki na wamerejea vyuoni kujiendeleza kielimu,” amesema Diamond, akisisitiza umuhimu wa mawasiliano mazuri kati ya wadau wa sekta ya habari na wasimamizi wa Sheria.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Wakili Patrick Kipangula, amesema Sheria ya Huduma za Habari ilitungwa mwaka 2016 na Serikali ilitoa kipindi cha mpito cha miaka mitano kwa waandishi na taasisi za habari kutimiza matakwa ya kisheria.

Ameeleza kuwa kipindi hicho kiliongezwa kwa miaka miwili na baadaye miaka mingine mitatu, hivyo kufikisha jumla ya miaka kumi, muda ambao Serikali inaamini ulikuwa wa kutosha kwa wadau wote wa sekta ya habari kujiandaa na kutekeleza Sheria hiyo kikamilifu.

Wakili Kipangula amesema utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari unalenga kujenga sekta ya habari yenye weledi, maadili na heshima, sambamba na kulinda maslahi ya waandishi, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment