December 13, 2025

MABAMBA- ATAKA TEMESA KUWA TAASISI YA MFANO KIUTENDAJI

Mameneja wa mikoa na vituo wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) nchini wametakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kubadilisha mitazamo ya watumishi na wanaopewa huduma na Wakala ili kuufanya kuwa mfano wa kuigwa na Taasisi zingine za Umma.
 
Hayo yamesemwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Moses R. Mabamba alipokuwa akizungumza na mameneja wa Mikoa na vituo katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Wakala mjini Dodoma ambapo amewaagiza mameneja hao kufanya kazi kwa bidii ili kutoa huduma bora kwa Serikali na jamii kwa ujumla ambazo zitaifanya TEMESA iweze kuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maslahi bora ya watumishi.
 
“Tufanye kazi tuzalishe, tulete hela tuwalipe watumishi, mfanyakazi ni rasilimali ya thamani kwenye Taasisi na ndiye ambaye anaifanya biashara yako ifanyike, tunahitaji kujenga taswira yetu nzuri ili kuwapa imani wateja wetu.” Ameongeza Mabamba.
 
Katika hatua nyingine, Kaimu Mtendaji Mkuu amewapa miezi mitatu watumishi wazembe ambao hawataki kufanya kazi kubadilika na amewapa miezi mitatu kuanzia sasa watumishi hao kubadilika ama la sivyo watafikiwa na kuchukuliwa hatua stahiki.
 
“Lakini wale walioshindikana kabisa mtanipa na mimi huwa sio muumini wa watu ambao hawataki kufanya kazi, ukiuliza mtu yoyote upande wangu mbaya huwa ni huo na napenda kuutekeleza kwa haraka sana, kwa hiyo wale watoboa mitumbwi tuwape muda kwanza wajibadilishe, tuwape miezi mitatu.’’ Amesema Mabamba.
 
Aidha, Mabamba amewaagiza mameneja hao kufikiria kibiashara kwakuwa maeneo mengi ya Wakala huo yanashawishi kufanyika kwa biashara kutoka vyanzo vingine na kuongeza kuwa faida kubwa ambayo TEMESA inayo ni kuwa na maeneo maeneo ya thamani yenye kushawishi ufanyikaji wa biashara.

No comments:

Post a Comment