December 08, 2025

JK AENDELEA KUWA KINARA WA ELIMU DUNIANI

Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) akiongea na wajumbe wa  Bodi ya GPE baada ya kumalizika kwa mkutano huo mjini Brussels, Ubelgiji. Pamoja naye ni Afisa Mtengaji Mkuu wa GPE, Bi Laura Frigenti
Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) akiteta jambo na Bi. Christine nHogan, Makama mwenyekiti wa GPE wakati wa mkutano wao mjini Brussels, Ubelgiji.
Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE)  akishiriki Mkutano wa 23 wa Kimataifa wa Qatar mjini Doha
Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) akiteta jambo na Dkt Hamad bin Abdulaziz Al Kawari, Waziri wa Nchi na Naibu Waziri Mkuu wa Qatar, mjini Doha leo. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe Habib Awesi Mohamed.
***************
Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) ameendelea na jitihada za kukuza elimu duniani.
 
Kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya GPE alisimamia Mkutano wa mwisho wa Bodi hiyo wa kuhitimisha Mpango wa 4 wa Miaka 5 wa Mzunguko wa Ufadhili wa GPE (4th financing campaign 2021 - 2025) ambao ulifanikiwa kukusanya takriban Dola za Kimarekeni bilioni 4.1 kwa ajili ya kugharamia uboreshaji wa elimu ya awali na ya msingi kwa watoto wanaoishi katika nchi za kipato cha chini na zinazoendelea, hususan watoto wa kike na wale wanaojikuta kwenye mazingira magumu kama vile ya vita, ukame, mafuriko, nk.
 
Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo uliofanyika wiki hii huko Brussels, Ubelgiji ulitathmini mkakati wa kukusanya fedha uliofanyika kwa mafanikio katika kukusanya fedha kupitia utaratibu wa misaada (grants) na ufadhili wa pamoja (co - financing) ambapo nchi zinazonufaika na miradi ya GPE huchangia kiasi cha fedha kwenye sekta ya elimu na GPE huongezea kiasi kinachobakia kwa makubaliano maalumu.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na GPE, kiasi hicho cha Dola za Marekani milioni 4.7 kilichopatikana kimesaidia kuboresha elimu kwa watoto takriban milioni 372 duniani kote huku watoto milioni 10 zaidi wakiandikishwa shule. Aidha, kupitia ufadhili wa GPE, walimu milioni 4.7 kote duniani walipatiwa mafunzo ya kuwaongezea ujuzi.
 
Aidha, Mkutano huo ulipokea taarifa ya mkakati wa utekelezaji wa mpango mpya wa 5 wa kampeni ya ufadhili wa GPE  utakaoanza mwaka 2026  hadi 2030. Kampeni hiyo imelenga kukusanya  Dola za Marekani milioni 5 na itaongozwa kwa pamoja kati ya Rais Bola Tinubu wa Nigeria na Waziri Mkuu Giorgia Meloni wa Italia.  Fedha zitakazopatokana kutokana na kampeni hiyo zitaongeza wigo wa GPE kuhudumia watoto takriban milioni 750 kote duniani kwa kuwapatia elimu bora zaidi inayoendana na mahitaji ya karne ya 21.
 
Vilevile, Mkutano huo ulishukuru baadhi ya nchi  ambazo zimeahidi kuendeleza ushirikiano na GPE kama vile Ujerumani ambayo tayari imeahidi kuchangia kampeni hii mpya ya GPE kiasi cha Dola za Marekani milioni 320 kwa kipindi cha miaka 6 ijayo.
 
Kwa kuzingatia mabadiliko ya sasa ya hali ya kifedha duniani ambapo wafadhili mbalimbali, hususan nchi zilizoendelea, zinabadilisha vipaumbele vyao vya maeneo ya kuelekeza ufadhili, Taasisi ya GPE imelenga kuendelea kuhakikisha inasimamia na kutumia vizuri fedha zinazotolewa na wafadhili ili kuwanufaisha watoto wengi zaidi duniani.

Vilevile,  GPE imepanga kuendelea kuzishawishi nchi ambazo siyo wafadhili waliozoeleka wa GPE (non traditional donors) kama vile nchi za mashariki ya kati ili ziweze kuoanisha programu zao za kusaidia elimu duniani na zile za GPE, na kuongeza fedha zaidi wanazochangia kwa GPE.
 
Kama sehemu ya kutekeleza mkakati huo, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya GPE Dkt. Kikwete  leo amepata fursa ya kushiriki Mkutano wa 23 wa Kimataifa wa Qatar  ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza utayari wa GPE kuendelea kushirikiana na Serikali ya Qatar katika jitihada zake za kusaidia watoto wenye mahitaji mbalimbali ya kielimu kote duniani.
 
Aidha, katika mazungumzo yake na Viongozi mbalimbali wa Taifa la Qatar pambezoni mwa Mkutano huo ameeleza nia ya GPE amepongeza mchango mkubwa wa Qatar katika elimu duniani na kuihakikishia utayari wa GPE kuendelea kushirikiana na Serikali ya Qatar na Shirika la Qatar la Education Above All Foundation.
 
GPE ni Taasisi iliyoanzishwa na Kundi la Nchi zenye Uchumi na Utajiri Mkubwa Duniani (G7) mwaka 2002 ili kuharakisha ufikiwaji wa lengo la elimu la kuhakikisha kila mtu, bila kujali umri, jinsia au hali ya kijamii, anapata elimu ya msingi bila malipo na kwa usawa. 

Tanzania ni moja ya nchi 90 zinazonufaika na miradi inayotekelezwa na GPE ambapo tangu ilipojiunga mwaka 2013 imeshapokea zaidi ya misaada yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 344 kusaidia jitihada zinazofanywa na Serikali kuendeleza elimu ya awali na ya msingi.

No comments:

Post a Comment