December 22, 2025

DKT. MWIGULU ATOA SIKU SABA KWA TANROADS, TARURA LINDI



WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa siku saba kwa Mameneja wa TANROADS na TARURA wa Mkoa wa Lindi wakae na kutafuta suluhisho la ujenzi wa daraja katika eneo la Congo kwenye barabara inayoenda Masasi kutokea Nachingwea.

Ametoa agizo hilo jana (Jumapili, Desemba 21, 2025) wakati akizungumza na viongozi na wananchi wa Nachingwea mara baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.

“Mje na suluhisho katika hili daraja la dharura. Kuanzia kesho wekeni mpangokazi wa kuokoa hiyo hali. Mkuu wa Mkoa wakupe taarifa kwamba wameshakaa, wamepanga nini na gharama zikoje. Fanyeni yote mawili hilo eneo la Congo na lile la stesheni,” alisema Waziri Mkuu.

“Barabara ilitengenezwa kwa dharura na sasa inatishia usalama wa wananchi. Kaeni na mwenzako wa TANRODS, mje na suluhisho. Wananchi wanataka wapite, wapitishe mazao yao. Fanyeni haraka, msisubiri tufike mahali watu hawapiti, ndiyo twende kulifanyia kazi. Wakati tunasubiri lami hiyo barabara lazima ipitike. Na ndiyo maana ninyi mko huku,” alisema.

Alikuwa akijibu maombi ya Mbunge wa Nachingwea, Bw. Fadhili Liwaka ambaye alimuomba Waziri Mkuu amsaidie ili eneo hilo korofi lisilete madhara kwa wananchi pindi mvua zikizidi. Aliomba pia eneo la Stesheni katika mji wa Nachingwea yawekwe makalavati ili kuepusha mafuriko katika eneo hilo.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu amejitahidi kuhakikisha nchi yetu ina barabara za kuunganisha mkoa na mkoa, na sasa tuko katika hatua ya kuunganisha wilaya kwa wilaya. Hapa kwetu, tuna barabara ya Masasi-Nachingwea ambayo inakidhi sifa zote mbili kwa maana ya kuunganisha wilaya lakini pia mikoa ya Lindi na Mtwara,” alisema mbunge huyo.

Alisema kwa niaba ya wananchi wa Nachingwea, anaomba barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami na kwamba wako tayari kupokea kilometa 20 katika kila mwaka ili kuwe na barabara za uhakika.

Aidha aliomba asaidiwe kupata minara ya mawasiliano katika eneo la Kilimarondo kwani wanazalisha korosho nyingi, wana fedha za kuweka benki na kuzitoa kwa kutumia mitandao ya simu.

Akijibu maombi hayo, Waziri Mkuu alisema barabara iliyotajwa iko kwenye Ilani ya Uchaguzi na kuhusu minara ya simu alisema analibeba ili kwenda kulifanyia kazi.

No comments:

Post a Comment