Wanamichezo kutoka klabu mbalimbali zinazoshiriki michezo ya 39 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) kesho tarehe 6 Septemba, 2025 watachuana katika mbio za kuendesha baiskeli kwa wanawake na wanaume.
Katibu Mkuu wa SHIMIWI, Bw. Alex Temba amesema mbio hizo, kwa wanaume zitakuwa kilometa 50, zitakanzoanzia Makaburi ya MV Bukoba eneo la Igoma hadi Nyanguge na kurudi walipoanzia.
Bw. Temba amesema mbio za wanawake zitakuwa Kilometa 30 na zitaanzia Makaburi ya MV Bukoba eneo la Igoma hadi Isangijo nakurudi walipoanzia.
Kwa kawaida mbio hizo zinafanyika kwa siku moja, na washindi wanazawadiwa kombe na medali kwa mshindi wa kwanza hadi wa tatu kwa wanawake na wanaume.
Katika hatua nyingine michezo ya kukamilisha ratiba ya makundi imefanyika leo kwa upande wa wanawake timu ya Wizara ya Uchukuzi wamewavuta Tume ya Utumishi mivuto 2-0; Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wamewashinda Wizara ya Madini kwa mvuto 1-0; Ofisi ya Bunge wamewashinda Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kwa mvuto 1-0.
Michezo mingine timu ya Tume ya Sheria waliwavuta RAS Pwani kwa mvuto 1-0; huku Wizara ya Mambo ya Ndani waliwashinda Wizara ya Maji kwa mivuto 2-0 na RAS Geita waliwashinda Wizara ya Mawasiliano kwa mivuto 2-0.
Katika mchezo wa mpira wa netiboli timu ya Maendeleo ya Jamii waliwafunga Tume ya Utumishu jwa 39-11; huku Bunge wakiwacharaza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa 33-21; nao Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa waliwafunga Wizara ya Uchukuzi kwa magoli 37-18; huku Ofisi ya Rais Ikulu wakipata ushindi wa chee wa magoli 40 na pointi mbili baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani kutoonekana uwanjani.
Katika michezo mingine ya netiboli timu ya Hazina wakiwafunga RAS Singida kwa magoli 20-18; nao Wizara ya Kilimo wakitakata mbele ya RAS Shinyanga kwa kuwafunga magoli 19-17; huku Ofisi ya Ukaguzi ya Taifa waliwaliza Uwekezaji kwa magoli 26-24; na Mahakama waliwachapa RAS Katavi kwa magoli 43-11.
Katika mchezo wa mpira wa miguu uliochezwa kwenye uwanja wa Nyamagana timu ya Wizara ya Maji waliwashinda Wizara ya Mambo ya Ndani kwa magoli 5-0; huku Wizara ya Ulinzi walitoshana nguvu na Wizara ya Ardhi kwa kutoka sare ya magoli 3-3; nao Wizara ya Viwanda na Biashara walitoka sare dhidi ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa magoli 2-2.
Mechi zilizofanyika kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya wavulana ya Bwiru, timu ya RAS Mwanza waliwashinda Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa magoli 2-1; huku Wizara ya Ujenzi wakitoshana nguvu na TAKUKURU kwa kutoka suluhu; kwenye uwanja wa Sabasaba timu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa waliwafunga ndugu zao Ofisi ya Bunge kwa magoli 2-0; na uwanja wa Mabatini timu ya Ofisi ya Maadili iliwafunga Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi kwa magoli 2-1; huku Uchukuzi wakiwafunga RAS Manyara kwa 4-0 na Umwagiliaji waliwafunga Makamu wa Rais kwa 3-2.








No comments:
Post a Comment