Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete ameipongeza Menejimenti na watumishi wa Ofisi hiyo kwa ushirikiano uliofanikisha Serikali ya Awamu ya Sita kupata mafanikio katika sekta za Kazi, Vijana, Ajira, Watu wenye Ulemavu na kinga ya Jamii.
Ameeleza mafanikio hayo wakati
wa kikao cha pamoja na watumishi wa Ofisi hiyo leo Agosti 21, 2025 ikiwa na
lengo la kuwashukuru watumishi na kuwapongeza kwa kutekeleza shughuli kwa ufanisi na tija
katika kipindi chote alicho hudumu na kuiongoza Ofisi.
Mheshimiwa Ridhiwani amesema
kuwa katika miaka minne ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Ofisi imepata mafanikio makubwa ikiwemo kupunguza kodi
ya mishahara kutoka asilimia 18 hadi 9, kutoa vibali 55,642 kwa wageni
waliokuja kufanya kazi na kupunguza muda wa utoaji wa vibali vya kazi kutoka
miezi miwili hadi siku 14.
Mafanikio mengine, Ofisi
imefanikiwa kutoa mikopo nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana yenye
thamani ya shilingi bilioni 3.2 kwa zaidi ya vijana 164,000, Serikali imezalisha
ajira zaidi ya milioni 8 kupitia miradi ya Bomba la Mafuta, Reli ya Kisasa
(SGR) na bwawa la Nyerere. Vilevile, Serikali imefanikiwa kupandisha pensheni
ya chini kutoka shilingi 100,000 hadi 150,000 kwa mwezi.
Mheshimiwa Ridhiwani ameeleza
mafanikio mengine kuwa ni kuwapeleka watanzania 7,907 kwenye ajira nje ya nchi
na kutoa mafunzo ya uanagenzi kwa vijana 121,526 katika sekta za kilimo, TEHAMA
na ujenzi, na mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa vijana 22,176 kupitia utarajali.
“Mafanikio yaliyopatikana si
ya Taasisi peke yake bali ni ya kila mtumishi aliyehusika kwa namna moja au
nyingine” alisisitiza Waziri Kikwete na kuongeza kuwa watumishi waongeze
ubunifu, matumizi ya TEHAMA, uwazi na uwajibikaji wa hali ya juu kwa manufaa ya
Taifa.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mary Maganga akizungumza
kwenye kikao hicho amesema Ofisi hiyo imefanikiwa kuandaa nyaraka mahsusi za
utendaji kazi ikiwemo Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya (2007), Toleo la
mwaka 2024; Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya mwaka 2023 pamoja na mkakati
wake;; Mpango kazi wa Taifa Haki na Ustawi kwa Watu Wenye Ualbino 2024/2025 –
2028/2029 (MTHUWWU);Mpango maalum wa Vifaa Saidizi (NATS)
Ameongeza kuwa, Miongozo na
mifumo mingine ni Mwongozo wa Uratibu wa Vyama vya Watu Wenye Ulemavu; Mwongozo
wa Majadiliano baina ya Serikali, Vyama vya Wafanyakazi na Vyama vya Waajiri, Mwongozo
wa Wakala Binafsi wa Ajira; Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za soko la Ajira, Mfumo
wa uratibu wa Kinga ya Jamii 2025 na Mfumo wa Kitaifa wa Kielektroniki wa
Taarifa za Soko la Ajira.
No comments:
Post a Comment