August 22, 2025

AMANI IWE SILAHA YETU KUELEKEA UCHAGUZI-TUNDUMA-SONGWE

Na Issa Mwadangala.
Wananchi wa Mtaa wa Unyamwanga Mji wa Tunduma Wilaya ya Momba Mkoani Songwe wamejengewa uelewa kuhusu madhara ya kufanya vurugu na uchochezi katika kipindi cha uchaguzi, sambamba na kusisitizwa umuhimu wa kudumisha amani katika jamii kwa maendeleo ya taifa letu.

Akizungumza Agosti 21, 2025 na wakazi wa eneo hilo, Polisi kata ya Tunduma Mkaguzi wa Polisi  Yahaya Mkwama amewaasa wananchi kutokubali kutumiwa na watu wenye nia ovu kuvuruga hali ya usalama, akibainisha kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

"Katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi, ni muhimu kila mmoja wetu awe mlinzi wa amani, tusikubali kuchochewa au kutumbukia kwenye vurugu ambazo mwisho wake huleta majuto. Jeshi la Polisi tupo kwa ajili ya kulinda usalama wa kila raia bila upendeleo," amesema Mkaguzi Mkwama.

Pia, Mkaguzi Mkwama, alisema Jeshi la Polisi linahakikisha jamii inapata uelewa sahihi kuhusu nafasi yao katika kulinda amani, hasa nyakati za uchaguzi ambazo mara nyingine hutumiwa vibaya na baadhi ya watu kusababisha uvunjifu wa sheria katika jamii kitendo ambacho si sawa.

Mkaguzi Mkwama alihitimisha, kwa kuwaeleza wananchi hao kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuwahamasisha wananchi nchini kote kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, utulivu na heshima kwa kufuata sheria za nchi.

No comments:

Post a Comment