March 12, 2025

Ujumbe wa Urusi Wajifunza Juhudi za Ufuatiliaji wa Kaboni Tanzania

Kamishna wa Uhifadhi, Profesa Dos Santos Silayo akizungumza na wageni hao kutoka Russia ambapo pamoja na mambo mengine alieleza umuhimu wa ushirikiano huo baina ya pande zote mbili.
Na Mwandishio Wetu, Morogoro
Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kilichopo katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) leo kimepokea ujumbe wa wataalamu kutoka Urusi, ikiwa ni sehemu ya Mpango wa Utafiti na Elimu kati ya Urusi na Tanzania unaoendelea.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Mkurugenzi wa NCMC, Dk. Deo D. Shirima, alieleza umuhimu wa kituo hicho katika kusaidia juhudi za Tanzania za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, akisisitiza haja ya kuimarisha ushirikiano katika ufuatiliaji wa kaboni na uendelevu wa mazingira.

Dk. Shirima alifafanua kuwa NCMC ilianzishwa mwaka 2016 kama mradi chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Norway na baadaye ikapokelewa rasmi na SUA mwaka 2018. Mwaka huu, kituo hicho kimepata kutambuliwa kisheria chini ya sheria ya mazingira ya taifa kama taasisi inayosimamia usajili wa kaboni na uandaaji wa hesabu ya gesi joto nchini, miongoni mwa majukumu mengine chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais (VPO).

Aliongeza kuwa kituo hicho kinafanya kazi kama mkono wa kiufundi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, hasa katika kusaidia wizara kutekeleza majukumu yake ya kuripoti kuhusu mabadiliko ya tabianchi chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC). Majukumu yake makuu ni pamoja na kuandaa hesabu ya kitaifa ya gesi joto, kusajili miradi ya kaboni, na kutekeleza mchakato wa Upimaji, Kuripoti, na Uhakiki (MRV).

“Hivi sasa, NCMC inasimamia miradi 72 ya kaboni katika hatua mbalimbali za usajili, ambapo miradi mingi inalenga masoko ya hiari ya kaboni. Takribani 32% ya miradi hii iko kwenye sekta ya misitu, 37% kwenye sekta ya nishati, huku mingine ikiwa kwenye kilimo, kilimo-misitu, taka, ardhi za malisho, na mifugo. 

Mchakato wa usajili unazingatia viwango vya kimataifa kama Verra Standard, Gold Standard, na Plan Vivo Standard,” alisema.

Dk. Shirima alisisitiza fursa za ushirikiano katika maeneo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuandaa viwango vya kitaifa vya MRV, kuboresha teknolojia za upimaji wa kaboni kupitia uchunguzi wa mbali, na kufanya tafiti kuhusu uzalishaji wa gesi chafuzi kutoka kwa sekta za kilimo, misitu, na mifugo. 

Pia alieleza fursa katika usimamizi wa taka na suluhisho endelevu za nishati kama vile biochar na mbolea za kikaboni, pamoja na kujenga uwezo wa kitaifa wa wataalamu.

Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, aliyekuwa akiongoza ugeni wa wataalamu hao, alisema wataalamu hao wamebobea katika utafiti wa kisayansi wa misitu na walijikita katika kuimarisha uhusiano wa kisayansi, kielimu na kiteknolojia kati ya Tanzania na Russia katika sekta ya misitu na uhifadhi wa mazingira. 

Alibainisha kuwa wataalamu hao watakuwa msaada mkubwa kwenye biashara ya kaboni kutokana na ubobezi walionao.

Wataalamu hao, walioongozwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Ufundi wa Misitu cha Jimbo la Saint Petersburg, Chuo Kikuu cha Petrozavodsk, na Chuo Kikuu cha Misitu na Teknolojia cha Jimbo la Voronezh, walilenga kuimarisha ushirikiano wa kisayansi na kielimu kati ya Tanzania na Urusi kwa madhumuni ya kuendeleza ufuatiliaji wa kaboni, utafiti wa mazingira, na miradi ya maendeleo endelevu.

No comments:

Post a Comment