February 14, 2025

WANANCHI WAASWA KUKOPA KWENYE VIKUNDI VILIVYOSAJILIWA

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Vijijini Bw. Shadrack Mhagama akizungumza na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi za Fedha (hawaonekani pichani) wakiwa ofisini kwake kabla ya kuanza kutoa Elimu ya Fedha katika Halmashauri ya Moshi Manispa, Mkoani Kilimanjaro.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Vijijini Bw. Shadrack Mhagama akizungumza na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi za Fedha wakiwa ofisini kwake kabla ya kuanza kutoa Elimu ya Fedha katika Halmashauri ya Moshi Manispa, Mkoani Kilimanjaro
Wanavikundi, Wajasiriamali Wadogowadogo, Wanasaccos, Wafugaji, Wakulima, Waendesha bajaji na bodaboda wakisikiliza mada mbalimbali zilizotolewa na Wataalamu wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na baadhi ya Taasisi za Fedha wakati wa semina ya Elimu ya Fedha iliyofanyika Kata ya Uru Mashariki Halmashauri ya Moshi Manispaa Mkoa wa Kilimanjaro.
Afisa Mwandamizi Masoko na Mawasiliano, kutoka Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga, akitoa elimu ya Uwekezaji uliopo UTT AMIS wakati wa Semina ya Elimu ya Fedha iliyofanyika katika Kata ya Uru Mashariki Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Vijijini Mkoa wa Kilimanjaro.
Wanafunzi wa Sekondari ya Mbokomu wakisikiliza mada mbalimbali zilizotolewa na Wataalamu wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na baadhi ya Taasisi za Fedha wakati wa semina ya Elimu ya Fedha iliyofanyika Shuleni hapo katika Kata ya Mbokomu Halmashauri ya Moshi Manispaa Mkoa wa Kilimanjaro.
Baadhi ya Wazazi wa Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mbokomu wakisikiliza mada mbalimbali zilizotolewa na Wataalamu wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na baadhi ya Taasisi za Fedha wakati wa semina ya Elimu ya Fedha iliyofanyika Shuleni hapo katika Kata ya Mbokomu Halmashauri ya Moshi Manispaa Mkoa wa Kilimanjaro.
****************
Na. Eva Ngowi, WF, KILIMANJARO
Serikali imewaasa wananchi kuepuka kukopa fedha kwenye Taasisi ama vikundi vinavyotoa huduma za kifedha bila kusajiliwa rasmi kwa mujibu wa sheria ili kuepuka athari zinazoambatana na mikopo umiza.

Tahadhari hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Vijijini Bw. Shadrack Mhagama, katika kikao kilichofanyika ofisini kwake alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi za Fedha walioko Mkoani Kilimanjaro, Wilaya ya Moshi Vijijini kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi.

Aidha, Bw. Mhagama aliwaasa wananchi wa Manispaa ya Moshi Vijijini hasa watoa huduma za fedha kuwa wahakikishe wanasajili biashara zao ili kuepuka kuwaumiza wananchi na mikopo kausha damu, na kuwataka pia wananchi waache kukimbilia huduma za haraka ambazo sio salama na kuwashauri kuwa kabla ya kuomba mkopo wahakikishe kuwa mkopeshaji yuko kihalali kwa mujibu wa sheria.

“Ni kweli kwa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi tunao watu ambao wanatoa huduma za kifedha lakini hawajasajiliwa; kwa kweli tunaweza kusema ni biashara haramu (illegal business) ambayo inafanywa nje ya utaratibu. Pia imebainika kuwa wananchi wengi wako katika vikundi ambavyo havijasajiliwa rasmi kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha ya mwaka 2018, kwa hiyo nitoe rai kwa wananchi ni vyema wakawa na mwamko wa kujiunga katika vikundi ambavyo ni rasmi na vimesajiliwa kwa mujibu wa Sheria hiyo.” Alisema Bw. Mhagama

Vilevile,  Bw. Mhagama alitoa rai kwa wananchi kwa kutoa taarifa kwa Mamlaka  husika watoe taarifa kwa Mamlaka husika ambazo ni pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii kwenye Mamlaka zao za Wilaya na Mikoa, watakapobaini kuna vikundi vya huduma ndogo ya fedha mitaani vinatoa Huduma za Fedha pasipo kusajiliwa. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionensia Mjema alisema kuwa Serikali inaendelea na program ya utoaji elimu hapa nchini na kwa sasa ni zamu ya Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo wananchi wamepata elimu namna wanavyoweza kuwa na nidhamu ya kujiwekea akiba lakini pia wamepata uelewa juu ya mikopo umiza ili kuepukana na changamoto hiyo kwa sasa ya mikopo kausha damu.

Awali, akizungumza katika semina hiyo Mkazi wa Kata ya Uru Mashariki, Halmashauri ya Moshi Vijijini, Bi.  Lusiana Mushi, alisema kuwa ujio wa Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi za Fedha umewafungua macho kuhusiana na akiba, vyama viwe vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria na sehemu salama ya kuweka fedha.

Aidha, Bw. Philbert Macha ambaye pia ni mwana kikundi kilichopo katika Kata ya Mbokomu, Halmashauri ya Moshi Manispaa alisema kuwa kupitia elimu aliyoipata amejifunza mengi na ataenda kuwaelimisha watu wengine maana anaona mikopo mingi inakopeshwa na watu binafsi na taasisi mbalimbali ambapo wengi wanakopa bila kuwa na malengo.

Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi za Fedha imefanikiwa kutoa elimu ya fedha katika Shule ya Sekondari Mbokomu, Vikundi vya wakina mama na wajasiriamali wadogo wadogo Kata ya Mbokomu na Wanakijiji wa Kata ya Uru Mashariki, Halmashauri ya Moshi Manispaa Mkoa wa Kilimanjaro.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Vijijini Bw. Shadrack Mhagama aliyevaa Kaunda suti nyeusi) akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Wataalamu wa kutoa Elimu ya Fedha, kutoka Wizara ya Fedha na baadhi ya Taasisi za Fedha, ambao watatoa elimu hiyo katika Halmashauri ya Moshi Manispaa, Mkoani Kilimanjaro.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini -WF - Kilimanjaro)

No comments:

Post a Comment