February 10, 2025

SIMULIZI ZA WANUFAIKA: VITUO VYA MFANO VINAVYOBADILI MAISHA YA WACHIMBAJI

Lwamgasa na Katente
Wanufaika wa Vituo vya Mfano vinavyotoa mafunzo ya uchimbaji na uchenjuaji bora wa  madini vya Lwamgasa- Geita na Katente-Bukombe wameonesha kuridhishwa na jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya uchimbaji mdogo, ikiwemo kuhamasisha matumizi ya  teknolojia bora za uchenjuaji  madini  ambazo  zimesaidia kuongeza ufanisi wa shughuli za uchimbaji mdogo  na uzalishaji.

Wazikungumza na Maafisa Habari kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini, waliotaka kufahamu ni kwa namna gani vituo hivyo vimewasaidia kuongeza tija katika shughuli zao.
Fortunatus Luhemeja, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hexad na mchimbaji mdogo,

Luhemeja amesema baada ya kupata taarifa za uwepo wa Kituo cha Mfano cha Lwamgasa alianza kutumia huduma kutoka kituoni hapo na hivyo kupelekea kupata uzalishaji mkubwa ukilinganisha na uzalishaji waliokuwa wakiupata awali.

Luhemeja ameongeza kwamba, baada ya kuanza kutumia Kituo cha Lwamgasa, kiliwaletea tija ndani ya muda mfupi kitu ambacho kiliwapelekea kuanza kutumia pia Kituo cha Katente na kuzidi kuona mafanikio na hivyo kupelekea kuwa na ujasili wa kuongeza uzalishaji na kuwekeza zaidi ambapo kwa sasa mafanikio ya uwepo wa Vituo hivyo kwenye uwekezaji wao yanayonekana.

‘’Tuliona mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi, na tukaongeza ujasiri wa kuongeza uzalishaji na kuwekeza zaidi," anasema Luhemeja, akipongeza ushirikiano wa STAMICO na wataalamu waliopo katika vituo hivyo kutoa miongozo ya kitaalamu.

Aidha, Luhemeja amesema, mbali na kupeleka mawe kwa ajili ya kuchakatwa katika Vituo hivyo, Wizara ya Madini kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ilipeleka  wataalamu kwa ajili ya ushauri na miongozo mbalimbali na kutokana na hali hiyo wakajikuta wakiupenda mfumo huo na kupelekea kuajiri wataalamu wao wakiwemo wahandisi, wanamazingira, wahasibu, maafisa  Rasilimaliwatu, wajiolojia na wataalamu wengine ambapo kwa sasa mafanikio na ufanisi wa kampuni hiyo unaonekana.

Pamoja na mambo mengine, Luhemeja amesema marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 yalimpelekea kuzipenda shughuli za Sekta ya Madini ambapo masuala mengi yamewekwa wazi huku upatikanaji wa masoko ya bidhaa zitokanazo na madini ukawa katika utaratibu mzuri kuliko ilivyo kuwa awali hivyo kupelekea kuhamasisha na kuingia katika shughuli za madini.

Luhemaja anamaliza kwa kunukuu maandiko kutoka kwenye Biblia akisema yanasema "watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa", na hivyo anatumia nafasi hiyo amewasihi watanzania wenye nia ya kufanya shughuli za uchimbaji akisema ‘’wasiogope kwasababu katika kipindi hiki maarifa yapo, masoko yapo,miongozo ipo, utaratibu upo na miundombinu ipo’’.





Christopher Kadeo –Mwenyekiti Mstaafu wa Wachimbaji Wadogo wa Madini wa Mkoa wa Geita

Kwa upande wake, Christopher Kadeo anasimulia kwamba yeye binafsi ana uzoefu wa zaidi ya miaka 40 katika uchimbaji wa madini na ana zaidi ya miaka 35 ya uchimbaji katika Kijiji cha Lwamgasa ambapo amesema ujio wa Kituo cha Mfano cha Lwamgasa kimemfanya afanikiwe katika shughuli zake za uchimbaji.

"Tunaishukuru Serikali yetu ambayo ni sikivu, tuliomba masoko tukaletewa, tukaomba tusogezewe ofisi ya upimaji madini tukaletewa GST, Serikali haikuishia hapo ikatuletea Vituo vya Mfano, imetuletea mashine ya uchorongaji (Drilling Rig) na imeendelea kuboresha mazingira na sasa tunapata mikopo katika taasisi za kifedha", anasema Kadeo.
 
Kadeo pia anasisitiza kuwa uchimbaji wa madini ni Sayansi, na siyo jambo la kishirikina kama wengi wanavyodhani. Amewashauri wachimbaji wengine kufika katika Vituo vya Mfano kujifunza teknolojia bora na mbinu sahihi za uchimbaji ili kufanikiwa zaidi na kuachana na mila potofu za kwenda kupiga ramli

Masunga Mashauri – Mchimbaji Mdogo wa Madini, Kijiji cha Lwamgasa
Naye, Masunga Mashauri ambaye ni Mchimbaji mdogo katika Kijiji cha Lwamgasa ameishukuru Serikali kwa kuwafungulia Kituo cha Mfano cha Uchenjuaji Lwamgasa ambacho kimemsaidia kwa kiasi kikubwa kupata mafanikio katika shughuli zake za uchimbaji.

Mashauri anasema gharama za uchenjuaji katika  vituo hivyo ni nafuu na  ameiomba Serikali kupitia STAMICO kukiongeza uwezo kituo hicho ili kiweze kuchakata mbale kwa wingi na kwa muda mfupi kuliko ilivyo sasa  kutokana na foleni ya mizigo inayongoja kuchakatwa.

No comments:

Post a Comment