Lengo kuu la mikopo hii ni kuwasaidia wananchi wa kundi hili kujikwamua kiuchumi na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika hafla hiyo, Moyo alisisitiza umuhimu wa kufuata kanuni za utoaji mikopo kwa kuhakikisha usawa, haki na ufanisi katika usambazaji wa fedha hizi. Alionya dhidi ya kurejesha mikopo kupitia njia zisizo rasmi kama vile ofisi za kata au maafisa maendeleo ya jamii, akisema kuwa mchakato wa kurejesha utahakikisha uwazi na utaratibu wa kisheria.
Mikopo hii imetolewa kwa awamu ya kwanza chini ya kaulimbiu "Pochi la Mama Limefunguka", ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kufanyika marekebisho kutokana na changamoto zilizojitokeza mwaka 2023 kama vile vikundi hewa na kushindwa kwa baadhi ya vikundi kurejesha mikopo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nachingwea, ndugu Joshua Mnyang’ali, alielezea kuwa vikundi 33 vya wanawake vimepata Shilingi Milioni 365, vikundi 22 vya vijana vimepata Milioni 375, na vikundi 5 vya walemavu vimepata Milioni 60. Alisema kwamba usimamizi mzuri wa mikopo ni muhimu ili kuhakikisha inarejeshwa kwa wakati na faida inapatikana kwa wote.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Adinan Mpyagila, alikumbusha wanufaika kutimiza majukumu yao kwa kutumia mikopo kwa malengo yaliyoainishwa na kurejesha kwa wakati ili kuwezesha wanufaika wa awamu zijazo kupata mikopo hiyo kwa urahisi.
Wanufaika wa mikopo hiyo walishukuru Serikali kwa msaada huo na walieleza kujitolea kwao kurejesha mikopo kwa wakati ili wafaidi wengine.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Halmashauri, wanufaika, na wadau wa maendeleo ya jamii.
No comments:
Post a Comment