Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt, Selemani Jafo,akizungumza na wananchi wakati wa zoezi la uzinduzi wa ulipaji fidia kwa wananchi wa eneo la Kata ya Engaruka Wilayani Monduli ili kupisha Mradi wa Magadi Soda.
Na.Mwandishi Wetu
SERIKALI imeagiza kuwa zoezi la ulipaji fidia ya sh, bilioni 6.2 kati ya sh, bilioni 14.48 kwa Wananchi 595 kutoka vijiji vinne vya Engaruka Chini, Mbaash, Idonyonado na Irerendeni. Kata ya Engaruka Wilayani Monduli kwa ajili ya kupisha Mradi wa Magadi Soda likamilike ifikapo Februari 15, 2025.
Akizungumza na Wananchi wa Eneo hilo Januari 2023 kwa niaba ya Rais Samia Hassan Suluhu wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo la ulipaji fidia , Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt, Selemani Jafo alisema fedha hizo za fidia zimetolewa ikiwa ni Mkakati wa kutekeleza Miradi huo wa Kielekezo wenye manufaa makubwa katika kuendeleza sekta ya viwanda, kuongeza ajira, kukuza Pato la Taifa na uchumi kwa ujumla.
Aidha, ameliagiza Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC ) kuhakikisha ulipaji huo unatetendeka kwa haki na kufuatilia malalamiko yote ya wananchi yakayojitokeza kushughulikiwa ipasavyo, kuandaliwa kwa mipango miji itakayoruhusu ujenzi wa hoteli na huduma nyingine za jamii huku akiwataka Wananchi kuchangamkia fursa zitakazojitokeza kupata ajira na na kuendeleza biashara.
Vilevile, alilisisitiza Shirika hilo kusimamia upatikanaji wa Wawekezaji wenye sifa na uwezo na si makanjanja ili Mradi huo ulete manufaa kwa Taifa na Wananchi kwa kurahisisha upatikanaji wa malighafi hiyo nchini na kuokoa fedha nyingi za kigeni zilizokuwa zinatumika kuagiza malighafi hiyo nje ya nchi.
Aidha amewasisitiza Wananchi kupuuza Taarifa potofu ambazo zimekuwa zikienezwa na watu ambao hawaitakii mema nchi yetu kwa kuwa NDC ambao ndio watekelezaji wa mradi huu wamekabidhiwa Cheti cha Ithibati za mazingira kutoka Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kinachothibitisha kuwa uchimbaji wa magadi soda katika Eneo la Engaruka hauna athari zozote za kimazingira kwa ndege ain flamingo ambao hawapo eneo hilo.
Dkt Jafo pia amebainisha kuwa Serikali imeweka mpango wa kukahakisha eneo la Engaruka barabara zake zinapitika pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa umeme mkubwa KV 33 kwa ajili ya kuendesha viwanda sanjari na upatikanaji wa huduma za kijamii katika sekta za elimu, afya na maji safi na salama.
Aidha, Viongozi mbalimbali walioshiriki Hafla hiyo wamesema kuwa Mradi hiyo uliosubiriwa kwa miak takribani 20 utakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo katika eneo hilo la Engaruka, Arusha na Taifa kwa ujumla.
Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda amesisitiza kuwa Wizara yake itashirikiana na Wananchi wa Wilaya za Longido na Monduli kuweka mipaka na kuwa na mipango bora ya matumizi ya Ardhi katika vijiji vya Engaruka ili kuepuka migogoro kwa kushirikiana na kamati za vijiji.
"Wananchi wasigombanishwe na migogoro ya mipaka kati ya Wilaya za Longido na Monduli wekeni mipaka ili maendeleo yapatikane na wizara hii itatoa ushirikiano saa zote na RC Makonda pale unapoona panakero tuwasiliane ili kutatua migogoro ili wananchi waishi kwa amani "
Vilevile, amewaelekeza Maafisa Ardhi katika Wilaya ya Monduli na Longido kushiriki kikamilifu katika zoezi la kurejesha mawe ya mpaka ya wilaya hizo mbili yaliyong'olewa na kupoteza utambuzi wa mpaka huo.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge , Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Ditopile aliipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kufanikisha jambo hilo lililokuwa na historia na fidia hiyo ilipwe kwa kuzingatia usawa na haki ili zoezi hilo lisiingie dosari kwa wananchi katika ulipwaji wa fidia.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda, amesema Arusha ni miongoni mwa mikoa yenye bahati na kadri siku zinavyosonga, Mkoa huu utatoa fursa mbalimbali za maendeleo kwenye sekta za Kilimo, Madini na Michezo, zitakazosaidia wananchi kujikwamua na umaskini akihimiza kuendelea kupewa kipaumbele cha ajira kwa wazawa wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye Mkoa wa Arusha.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo wa Kimkakati, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC Dkt.Nicolaus Shombe amesema Mradi huo wa Magadi Soda umechukua zaidi ya miaka 20 tangu mchakato wake ulipoanza baada ya NDC kufanya utafiti wake na kubaini uwepo wa magadisoda yenye kufikia mita za ujazo Bilioni 3.8 sawa na tani Milioni 787 ambapo kupitia utekelezaji wake, viwanda viwili vikubwa vitakavyogharimu Trilioni 1.6 vitajengwa katika eneo hilo lenye jumla ya ekari 60, 884.
Alisema viwanda mbalimbali zinatumia magadi soda hayo na Tanzania ni waagizaji wakubwa sana wa magadi soda hayo kutoka nchi za Boswana na maeneo mengine huku ikitumia fedha nyingi za kigeni kuagiza hivyo mradi huo unaenda kuhamisha fedha hizo badala ya kununua nje magadi hayo yatatokea Eneo la Engaruka.
Vilevile, alifafanua kuwa Elimu ya fedha imetolewa kwa wananchi waliopo eneo hilo huku wananchi waliolipwa fidia wanapashwa kuondoka katika eneo hilo ndani ya siku 90 zijazo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mhe.Fredrick Lowassa alisema kuwa Wananchi wananyuso za furaha kutokana na fidia hii nakuiomba Seriiali kushughulikia changamoto za miundombinu zilizopo.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt, Selemani Jafo,akizungumza na wananchi wakati wa zoezi la uzinduzi wa ulipaji fidia kwa wananchi wa eneo la Kata ya Engaruka Wilayani Monduli ili kupisha Mradi wa Magadi Soda.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda,akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wa eneo la Kata ya Engaruka Wilayani Monduli ili kupisha Mradi wa Magadi Soda.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda,akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wa eneo la Kata ya Engaruka Wilayani Monduli ili kupisha Mradi wa Magadi Soda.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge , Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Ditopile,akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wa eneo la Kata ya Engaruka Wilayani Monduli ili kupisha Mradi wa Magadi Soda.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah ,akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wa eneo la Kata ya Engaruka Wilayani Monduli ili kupisha Mradi wa Magadi Soda.
Sehemu ya wananchi wakimsikiliza Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt, Selemani Jafo (hayupo pichani) ,akizungumza na wananchi wakati wa zoezi la uzinduzi wa ulipaji fidia kwa wananchi wa eneo la Kata ya Engaruka Wilayani Monduli ili kupisha Mradi wa Magadi Soda.
No comments:
Post a Comment