January 16, 2025

TCAA YAWASILISHA MIKAKATI YA KUIMARISHA SEKTA YA ANGA KWA KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU





Na Mwandishi Wetu, TCAA
MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imejipanga kutekeleza mikakati yenye lengo la kuhakikisha kunakuwa na uendelevu wa kusimamia Sekta ya Usafiri wa Anga nchini kwa sasa na baadaye.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Salim Msangi wakati akiwasilisha mikakati hiyo mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu Januari 15, 2024 mkoani Dodoma.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuendelea kusimamia sheria na kanuni za usafiri wa Anga ili kuhakikisha Anga la Tanzania linaendelea kuwa Salama na kuwa kivutio kwa mashirika ya ndege ya kimataifa mbalimbali.

Kuendelea kufanya maandalizi kwa ajili ya Ukaguzi wa Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) ambapo kwa sasa TCAA imeendelea kuhuisha kanuni za usafiri wa Anga ili ziendane na matakwa ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani, kuhuisha nyaraka na miongozo ya wakaguzi ili ziendane na mabadiliko ya kanuni mpya. 

Mingine ni kuendelea kutoa mafunzo kwa ajili ya wakaguzi ili kupata weledi na namna bora ya kufanya kaguzi na usimamizi wa uthibiti wa Usafiri wa Anga na kuendelea kufanya kaguzi za ndani ili kutathimini uwezo wa kampuni zilizosajiliwa nchini kwa kuzingatia matakwa ya kanuni za Usafiri wa Anga nchini.

Mikakati mingine ni kuendelea kusimamia mafunzo endelevu kwa marubani, wahandisi, na watendaji wengine wa Sekta ya Usafiri wa Anga.

Pia kuendeleza uwekezaji katika mifumo ya kisasa ya uongozaji wa Ndege na mawasiliano kuhakikisha inaendana na mabadiliko ya kiteknolojia na matakwa na miongozo ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO);

Pia kuendelea kushirikiana na nchi jirani na mashirika ya kikanda na kimataifa kwa kushiriki mikutano na makongamano kwa lengo la kubadilishana uzoefu. 

Kuhimiza matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira katika Sekta ya Usafiri wa Anga kwa lengo la kupunguza athari za mazingira zinazotokana na shughuli za Anga.

Kuhakikisha viwanja vya ndege na miundombinu inayohusiana inakidhi viwango vya kimataifa.

Kuendelea kukitangaza chuo cha usafiri wa anga (CATC) ili kuweza kuwavutia watanzania na wasio watanzania kujiunga na masomo ya muda mfupi katika sekta ya Usafiri wa Anga.

Na kuendelea na ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga ili kuweza kuwa na mazingira bora zaidi ya kufundishia pamoja na vifaa vya kisasa.

Kamati imesisitiza kusimamia mikakati hiyo na kuhakikisha chuo cha CATC kinajengwa.

No comments:

Post a Comment