January 08, 2025

RAIS SAMIA AGUSWA NA KIFO MWENYEKITI WA CCM LIWALE.





Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesikitishwa na Kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Liwale Ndugu. Kindamba Milingo.
 
Akiwasilisha salamu za Chama cha Mapinduzi kwa waombolezaji waliojitokeza katika Msiba huo Uliofanyika leo (Jumatano, Januari 08, 2025) Nyumbani kwa Marehemu Pulipwite Liwale Mjini mkoani Lindi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais anatambua mchango mkubwa uliofanywa na marehemu enzi ya uhai wake katika kukijenga Chama cha Mapinduzi.
 
"Kwa niaba ya Mwenyekiti wetu wa Chama, Katibu Mkuu na viongozi wengine naomba kuwasilisha salamu za rambirambi kutoka Chama cha Mapinduzi CCM, viongozi wetu hawa wote wameguswa na kifo cha Milingo na wanatambua kazi kubwa aliyoifanya katika kukijenga chama kwenye ngazi ya Wilaya alipokuwa anahudumu”
 
Amesema marehemu mzee Milingo alikuwa kiunganishi kikubwa kati ya Chama na Serikali katika kuhakikisha wanafuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ili kusaidia kuongeza kasi ya maendeleo ndani ya Wilaya ya Liwale.
 
Mheshimiwa Majaliwa amesema ni vyema wanachama wa CCM wakaendelea kuenzi mazuri yote yaliyofanywa na Mwenyekiti huyo pamoja na kuendelea kumuombea.
 
"Mzee wetu amefanya kazi kubwa ndani ya chama, yeye pamoja na viongozi wengine walikiunganisha Chama na  Mkoa wa Lindi.
 
Naye Mbunge wa Liwale Zuberi Kuchauka amesema Wilaya ya Liwale imepoteza kiongozi Mahiri na Mwanachama Mtiifu wa Chama cha Mapinduzi  ambaye alijitoa kwa nguvu zote kukijenga chama hicho.
 
Marehemu Mzee Milingo alifariki tarehe 6 Januari 2025 katika hospitali ya Rufaa ya Sokoine Mkoani Lindi, amezikwa katika makaburi ya Nanganda Liwale Mkoani Lindi.

No comments:

Post a Comment