Na Mwandishi Wetu.
Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameonya vikali wakandarasi wazembe wanaochelewesha miradi ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia ucheleweshaji wowote ambao unakwamisha maendeleo na kuhatarisha maisha ya wakazi wa Dar es Salaam.
“Nataka ndani ya siku tatu ujenzi uanze usiku. Nitakuja hapa mwenyewe Alhamisi kuangalia kama kazi zinaendelea. Kama vinginevyo, hatua kali zitachukuliwa. Katibu Mkuu wangu na Mtendaji Mkuu wa Tanroads wasimamie hili,” amesema Waziri Ulega wakati wa ziara yake leo Jumapili, Desemba 15, 2024.
Amesema kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha miradi mikubwa ya miundombinu kama BRT inakamilika kwa ubora na kwa wakati ili kupunguza adha za foleni jijini Dar es Salaam. Waziri ameagiza wakandarasi kuzingatia mikataba yao na kufungua barabara wanapomaliza ujenzi ili kupunguza usumbufu kwa wananchi.
“Tunaelewa changamoto zinazotokana na ujenzi wa barabara hizi, lakini tunawaomba wananchi wavumilie. Changamoto za sasa ni neema kwa kesho baada ya kukamilika. Hii hadha ya leo itakuwa kicheko cha kesho,” amesema Ulega.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akitoa maelekezo kwa viongozi wa TANROADS walioambatana nae katika ukaguzi wa miundombinu.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Miradi ya BRT kutoka Tanroads, Mhandisi Frank Mbilinyi amesema mradi wa awamu ya tatu wa BRT unaogharimu Sh230 bilioni umefikia asilimia 72 na unatarajiwa kukamilika Machi 2025, huku miradi mingine ikiwa kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
Waziri Ulega ameahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote na kuhakikisha wakandarasi wazawa wanalipwa madeni yao kwa wakati, huku akisisitiza kuwa wakandarasi wanaofanya kazi kwa viwango watapewa kipaumbele katika miradi ijayo.
No comments:
Post a Comment