December 04, 2024

TUMIENI MFUMO WA e-ARDHI KIKAMILIFU-WAZIRI NDEJEMBI






Na Mwandishi wetu, Dodoma
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka watendaji wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha wanatumia mfumo wa ardhi Kidigitali ( e- Ardhi)kikamilifu kwa maeneo ambayo mfumo huo umeanza kutumika.

Mhe Ndejembi amesema hayo leo tarehe 3 Desemba 2024 jijini Dodoma wakati akizindua  rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi yatakayofikia kilele chake  siku ya Alhamisi desemba 5 , 2024.

Amemuelekeza katibu Mkuu wa wizara hiyo ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga kuchukua hatua madhubuti  kwa watumishi wa sekta ya ardhi wasiotaka kutumia mfumo huo kwa makusudi kwenye maeneo ambayo mfumo huo umeanza kutumika.

Kwa mujibu wa Mhe. Ndejembi, matumizi ya teknolojia siyo hiari kwa kuwa kupitia mfumo huo wa e-ardhi huduma za sekta ya ardhi zitaboreshwa na kuweza kuwafikia wananchi wengi wakiwemo wale wa vijijini.

Mfumo wa e-Ardhi tayari umeanza kutumika kwenye wmaeneo mbalimbali nchini kama vile Dodoma, Arusha, Tabora katika halmashauri ya Nzega, Pwani halmashauri ya Chalinze pamoja na manispaa ya Shinyanga na Kahama zilizopo mkoa wa Shinyanga.

Akigeukia suala la utendaji kazi wa watumishi wa sekta ya ardhi, Mhe Ndejembi amesema anaelewa kazi kubwa na nzuri wanayofanya watumishi wa sekta hiyo. Hata hivyo, amesema wapo watumishi wachache wanaotaka kuharibu sura nzuri ya wale watumishi wamaofanya kazi kwa bidii.

"Wale wanaofanya kazi kwa mazoea wizara haitawavumilia maana kitu cha kwanza anachokutana nacho mwananchi katika  ofisi za ardhi ni migogoro ya ardhi hivyo nataka tutoke huko" amesema Mhe. Ndejembi.

Aidha, amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kuboresha utendaji wao wa kazi kwa kufuata maadili na taaluma zao kwa kuwa wao ni kioo na pale wanapofanya jambo baya wanaichafua wizara pamoja na serikali nzima.

Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewahimiza watumishi wa sekta ya ardhi kusimamia vizuri mipango miji iliyopo na kuepuka ubadilishaji matumizi kiholela jambo alilolieleza linachafua miji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava amesema Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inatekeleza vyema miradi ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha (KKK) pamoja na Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP).

Aidha, Mhe. Mzava amesema baada ya maadhimisho hayo Bunge linatarajia sekta ya Ardhi itakuwa na mafanikio makubwa katika kuwahudumia wananchi ikizingatiwa kuwa, watumishi wa Sekta ya Ardhi ambao wanashiriki maadhimisho hayo wanatoka katika mikoa na halmashauri zote nchini.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaadhimisha Wiki ya Ardhi  kuanzia tarehe 2 hadi 5 Desemba 2024 ambapo mbali mambo mengine wiki hiyo inatumika kujadili utoaji huduma za kisekta pamoja na uwepo mawasilisho mbalimbali  kwa lengo la kufanya maboresho ya maeneo yenye changamoto.

No comments:

Post a Comment