December 12, 2024

TIMU YA MAJADILIANO YA MRADI WA LNG YAFANYA ZIARA YA MAFUNZO NCHINI INDONESIA


Timu ya Serikali ya Majadiliano ya Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (Government Negotiation Team – GNT-LNG) ipo katika ziara nchini Indonesia. 

Ziara hiyo inalenga kubadilisha uzoefu na ujuzi katika kuendeleza sekta ya ndogo ya mafuta na gesi asilia pamoja na kukuza ushirikiano baina ya nchi mbili katika sekta husika. 

 Ziara hiyo inaratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na inaongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio.

Katika ziara hiyo Dkt. Mataragio ameambatana na wajumbe wa GNT-LNG akiwemo Ndg. Elijah Mwandubya Naibu Katibu Mkuu – Wizara ya Fedha, Ndg. Nehemia Mchechu, Msajili wa Hazina, Ndg. Godluck Shirima, Kamishna wa Petroli na Gesi (Katibu wa GNT-LNG) na, Mha. Charles Sangweni ambaye ni Mwenyekiti wa GNT-LNG. 

Katika ziara hiyo, pamoja na masuala mengine, GNT imefanya mazungumzo na uongozi wa Wizara na Taasisi mbalimbali zinazosimamia sekta ya mafuta na gesi asilia nchini Indonesia ikiwemo Wizara inayosimamia masuala ya Uchumi na Uwekezaji, Wizara ya Rasilimali za Nishati na Madini (Ministry of Energy and Minerals Resources), Kampuni ya Mafuta ya Taifa ya nchini Indonesia (PERTAMINA) pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa shughuli za mkondo wa juu wa Petroli (SKK Migas). 

Mazungumzo hayo, pamoja na masuala mengine, yamejikita katika kuona namna ya kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo pamoja na kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa miradi ya LNG kwa kuzingatia uzoefu uliopo nchini Indonesia katika kutekeleza miradi ya namna hii. 

Aidha, GNT ilieleza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini katika sekta ya mafuta na gesi asilia na Indonesia wameonesha utayari wa kuendelea kushirikiana katika kuimarisha sekta husika. 

Akizungumza katika vikao vinavyoendelea, Dkt. Mataragio ameeleza nia ya kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Nishati ya Tanzania na Wizara ya Rasilimali za Nishati za Madini ya Indonesia. Aidha, Dkt. Mataragio alieleza kuwa Serikali za nchi hizo mbili zitaendelea kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Taasisi zinazosimamia rasilimali ya mafuta na gesi, ikiwemo PURA ya Tanzania na SKK Migas, vilevile kati ya TPDC na PERTAMINA. 

Katika ziara hiyo ya mafunzo, wajumbe wa GNT watatembelea mitambo mikubwa miwili inayozalisha LNG nchini Indonesia ambayo ni Botang LNG Plant na Donggi Senoro LNG Plant.


No comments:

Post a Comment