December 31, 2024

MIKOA YA RUVUMA, NJOMBE, SONGWE NA RUKWA KUBORESHA DAFTARI LA WAPIGA KURA JANUARI, 2025.












Mwandishi Wetu, Ruvuma
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza ratiba ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye mikoa ya Ruvuma, Njombe, Songwe na Rukwa ambapo zoezi hilo litafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 12 hadi 18 Januari, 2025.

Hayo yameanishwa kwenye hotuba ya Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jacobs Mwambegele iliyosomwa kwa niaba yake kwenye mikutano  ya Tume na  wadau wa uchaguzi iliyofanyika leo tarehe 31 Desemba, 2024 kwenye  mikoa ya Ruvuma, Njombe, Songwe na Rukwa.

Mhe. Mwambegele ambaye aliwakilishwa na wakurugenzi mbalimbali wa Tume kwenye mikutano hiyo,  amesema mikoa hiyo itafanya uboreshaji kwenye mzunguko wa tisa na kwamba tayari Tume imekamilisha uboreshaji kwenye mikoa 19 ambayo ilijumuisha mizunguko nane kati ya mizunguko 13 ambayo imepangwa kukabilisha zoezi hilo nchini.

“Leo tupo hapa Songwe na wenzetu wapo kwenye mikoa ya Njombe, Rukwa na Ruvuma ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye mkoa huu wa Songwe, Njombe, Rukwa na mkoani Ruvuma kwenye Halmashauri za Wilaya ya Nyasa, Mbinga, Mbinga Mji, Wilaya ya Songea na Manispaa ya Songea, zoezi litakalofanyika kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 12 Januari, 2025 na kukamilika tarehe 18 Januari, 2025 na ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni,” imesema sehemu ya hotuba hiyo.

Ameitaja mikoa ambayo tayari imekamisha zoezi hilo kuwa ni Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma na Singida.

“Mikoa mingine ni mikoa ya Zanzibar ambayo ni Mjini Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Arusha na Kilimanjaro. Kwa sasa mikoa miwili ya Mbeya na Iringa inatarajia kukamilisha zoezi hilo tarehe 02 Januari, 2025,” imesema sehemu ya hotuba hiyo.

Mada ya Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani iliyowasilishwa kwa niaba yake kwenye mikutano hiyo imeanisha kwamba kwenye mikoa hiyo jumla ya wapiga kura wapya 475,743 wanatarajiwa kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Mada hiyo imeanisha kuwa uboreshaji wa Daftari utakapokamilika, mikoa hiyo inatarajiwa kuwa na  jumla ya wapiga kura  3,091,485 ikilinganishwa na idadi ya wapiga kura 2,615,742 waliokuwemo kwenye Daftari mwaka 2020.

“Idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha,” imesema sehemu ya mada hiyo.

Mada hiyo imeanishwa kuwa kutakuwa na vituo 3,785 ikiwa ni ongezeko la vituo 233 kutoka vituo 3,552 vilivyokuwepo mwaka 2020.

No comments:

Post a Comment