Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametembelea banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakati akifunga Mkutano wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati 2024 uliofanyika leo tarehe 5 Disemba, 2024 jijini Arusha.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametembelea banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakati akifunga Mkutano wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati 2024 uliofanyika leo tarehe 5 Disemba, 2024 jijini Arusha.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema matumizi bora ya nishati yataziwezesha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kukuza uchumi ambao kwa kiasi kikubwa unategemea biashara na viwanda ambavyo navyo vinategemea nishati za aina mbalimbali.
Waziri Jafo ameyasema hayo leo Desemba 05, 2024 jijini Arusha wakati akifunga Mkutano wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati 2024 uliofanyika kwa siku mbili jijini humo.
Waziri Jafo ameishukuru Wizara ya Nishati kwa kuratibu mkutano huo kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa na Ubalozi wa Ireland ambao umewakusanya wataalam na wabobezi mbalimbali kwa ajili ya kubadilishana mawazo kuhusu matumizi sahihi ya nishati.
"Tumependekeza kuhakikisha matumizi sahihi ya nishati na jinsi gani tutalinda mahusiano kati ya jamii, wadau wa maendeleo ya nchi na nchi ili kwa pamoja tulete manufaa makubwa katika kuhakikisha matumizi sahihi ya nishati na muendelezo wa upelekaji nishati kwa wadau hususan kwa wananchi na viwandani", alisema Waziri Jafo.
Vile vile, amemshukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa anaoufanya katika upande wa nishati kwani uwekezaji huo unamaana kubwa katika ukuzaji wa biashara na viwanda.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amesema wizara imejipanga kuhakikisha inamuunga mkono Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo imeanza na kutunga Mkakati wa Matumizi Bora ya Nishati na kupitia mkakati huo, kila mwaka watakuwa wanatengeneza mipango ya maendeleo ya mwaka na kutenga bajeti ambazo zitasaidia kuhakikisha kwamba mkakati huo unatekelezeka na kuhakikisha wananchi wananufaika na matumizi bora ya nishati.
"Baadhi ya maazimio tuliyokubaliana ni kuhakikisha nchi zote za Afrika Mashariki na Ukanda wa SADC tunashirikiana katika kuendeleza teknolojia ya matumizi bora ya nishati na kufanya tafiti za pamoja kuboresha matumizi ya nishati. Pia, Sekta binafsi zitashirikishwa kikamilifu katika kuboresha matumizi ya nishati." Amemalizia Dkt. Mataragio.
No comments:
Post a Comment