Tundu Lissu, mmoja wa wanasiasa mashuhuri nchini Tanzania, ametangaza kwa msisitizo nia yake ya kuwania nafasi ya Uenyekiti wa CHADEMA Taifa.
Katika mkutano wake wa waandishi wa habari uliofanyika leo, Lissu aliweka wazi dhamira yake ya kurejesha umoja, mshikamano, na maridhiano ya kweli ndani ya chama na vyama vingine vya siasa nchini.
Lissu alieleza kuwa lengo kuu la uongozi wake litakuwa kuhakikisha kuwa CHADEMA inakuwa mfano wa kuigwa katika kukuza demokrasia na uwazi. Alisema kuwa ni muhimu kwa chama kujenga siasa za maelewano zitakazowezesha kufanikisha malengo ya mabadiliko ya kweli kwa Watanzania.
"Uongozi wangu utakuwa tayari kurudi kwenye maridhiano ya kweli. Tunahitaji siasa za kuelewana na mshikamano ili kufanikisha malengo yetu ya kuleta mabadiliko ya kweli kwa Watanzania," alisema kwa msisitizo.
Aidha, Lissu aliongeza kuwa, endapo atachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, atajitahidi kuhakikisha kuwa chama kinakuwa jukwaa lenye nguvu la kutetea haki za wananchi na kujenga siasa za mshikamano wa kitaifa. Alisema kuwa hatua hiyo itajumuisha kushirikiana na wadau wote wa kisiasa bila kujali tofauti zao kwa lengo la kuimarisha ustawi wa taifa.
Katika hotuba yake, Lissu pia alisisitiza umuhimu wa viongozi wa kisiasa kuweka mbele masilahi ya Watanzania kuliko masilahi ya kibinafsi. Aliahidi kuwa atafanya kazi kwa kushirikiana na wanachama wote wa CHADEMA ili kuimarisha chama na kuhakikisha kuwa kinaendelea kuwa sauti ya wanyonge nchini.
Mkutano huu wa Tundu Lissu unakuja wakati ambapo CHADEMA inajiandaa kwa uchaguzi wa ndani wa chama na huku mazingira ya kisiasa nchini yakiwa kwenye kipindi cha mabadiliko makubwa.
No comments:
Post a Comment