Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amesema wizara yake inaendelea kuboresha utoaji wa huduma za ardhi kwa wananchi ambapo mfumo wa e-Ardhi ndiyo suluhisho la migogoro ya ardhi nchini.
Waziri Ndejembi amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Novemba 21, 2024 katika Ofisi za Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma.
“Sisi tuna ‘digitalize’ kuondoa migogoro ya ardhi kwa wananchi wetu na kuhakikisha mifumo inasomana wakati wa kutoa huduma za ardhi, ujio wenu utasaidia kubadilishana uzoefu ili kuwahudumia wananchi wetu” amesema Waziri Ndejembi.
Akizungumzia suala la Kliniki ya Ardhi, Waziri Ndejembi amesema Wizara hizo mbili zitashirikiana katika zoezi la Kliniki ya Ardhi na kusisitiza kuwa Wizara yake ipo tayari kwenda Zanzibar na watumishi wa Ardhi Zanzibar kuja Tanzania Bara kubadilisha uzoefu ili kuleta tija katika kuwahudumia Watanzania kwa wakati.
“Tupo tayari kwa ushirikiano kwenye sekta ya ardhi, tufanye kazi kwa pamoja kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwa na taswira ya pamoja kimataifa” amesema Waziri Ndejembi.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhaza Gharib Juma amesema wanaendelea kupata ushirikiano mara zote kutoka Tanzania Bara kwenye sekta ya Ardhi.
Akitolea mfano amesema tayari makundi manne tayari yamekuja Tanzania Bara kujifunza wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambao walijifunza juu ya mifumo ya kutoa huduma za ardhi, kundi la pili ni ziara ya watendaji wa Wizara hiyo wakiongozwa na Katibu Mkuu Khadija Khamis Rajab ambao walitembelea Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya ambao walijifunza Mabaraza hayo yanavyofanyakazi.
Kundi la tatu ni watendaji wa Wizara hiyo wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu ambao wamejifunza utendaji wa Kituo cha Taarifa za Kijiografia (GIS) ambapo kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kituo cha Ubunifu na Mafunzo ya Teknolojia na Taarifa za Kijiografia (TNGC) tayari kimeanza kufanyakazi kwa ushirikiano na serikali ya Korea na kundi la nne watendaji wa Wizara hiyo wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Mhaza Gharib Juma ambao wamekuja kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa mwongozo wa Uthamini pamoja na mfumo wa Wathamini katika kutekeleza majukumu ya Uthamini.
Akiukaribisha ujumbe huo, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amesema ziara hiyo imekuja muda muafaka ambapo watabadilishana uzoefu kwa kila upande kutoa kizuri walichonacho ili kutekeleza majukumu yao kwenye sekta ya Ardhi nchini kwa tija.
No comments:
Post a Comment