November 24, 2024

WAONGOZA NDEGE WAPONGEZWA KWA UMAHIRI WAO WA UFANISI WA KAZI NCHINI

Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti Uchumi TCAA Bw. Daniel Malanga aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw.Salim Msangi akizungumza na wataalam wa Chama cha Waongoza Ndege Tanzania (TATCA) kuhusu namna Mamlaka hiyo ilivyojipanga kuwawezesha waongozaji ndege kufanya kazi kwa weledi na ufanisi wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 44 wa mwaka uliofanyika Novemba 22, 2023 jijini Dar es Salaam.


Na Mwandishi Wetu, TCAA
Tanzania imeelezwa kuwa na Wataalam wa kuongoza ndege nchini wenye umahiri mkubwa na kufanya huduma za usafiri wa anga nchini kuimarika na kuwa yenye idadi ndogo ya matukio.
 
Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Daniel Malanga wakati akifungua Mkutano wa 44 wa mwaka wa Chama cha Waongoza Ndege Nchini (TATCA), Novemba 22, 2024 jijini Dar es Salaam.
 
Bw. Malanga aliongeza kuwa umahiri huo unatokana na ukweli kwamba, wataalam hao wanaandaliwa hapa hapa nchini na kuongeza kuwa mbali ya wataalam hao kuwa mahiri pia TCAA imeendelea kuboresha mazingira yao ya kufanyia kazi ikiwemo kufunga mitambo ya kisasa ya radio za sauti inayorahisisha mawasiliano baina ya muongoza ndege na rubani.
                       
Aidha, Bw.Malanga amevutiwa na Kauli Mbiu  ya TATCA ya mwaka huu inayosema ‘Jenga Afya kwa Uongozaji Ndege wa ufanisi’, na kuwataka waongoza ndege hao licha ya kufanya kazi zao kwa umahiri pia wazingatie kulinda afya zao.
 
Mbali na ufunguzi wa Mkutano huo, Bw. Malanga pia alizindua Nembo mpya ya TATCA ambayo itatumika kutambulisha shughuli mbalimbali za uendeshaji wa chama hicho nchini.
 
Mkutano huo wa TATCA mbali na kuhudhuriwa na wanachama wa vyama rafiki vya hapa nchini, pia umehudhuriwa na wawakilishi wa vyama vya waongoza ndege kutoka nchi za Kenya, Uganda na Kongo DRC.
 
Kwa upande wake Rais wa TATCA,  Bw. Merkiory Ndaboya aliishukuru TCAA kwa kuendelea kuviwezesha vyama vya kitaaluma kuendelea kufanya kazi zao pamoja na mikakati ya TCAA ya kufunga mitambo ya kisasa ya radio za sauti ya kuongozea ndege inayowarahisishia utendaji kazi wao.

No comments:

Post a Comment