Mbunge wa Vijana Mkoa wa Ruvuma (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 24 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Kauli hiyo ameitoa Novemba 21, 2024 wakati wa uzinduzi wa Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma ambao unalenga kupata Viongozi wa ngazi za Mitaa, Vijiji na Vitongoji hapa nchini.
"Serikali kupitia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fedha ili kufanikisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule ya Wasichana, miradi ya kusambaza umeme kwenye Vijiji na Vitongoji, Elimu, Afya, Kilimo, Maji, Ujenzi wa Kituo cha Polisi na Mahakama katika wilaya hii ya Namtumbo." Ameeleza Mhe. Kapinga
Katika Sekta ya Umeme amesema kuwa, Vijiji zaidi ya 12,000 Tanzania Bara vimepata umeme na kazi hiyo imefanyika kwa mafanikio ikiwa ni maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Mhe. Kapinga amewaasa wananchi kuwa ifikapo Novemba 27, 2024 wajitokeze kwa wingi kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na wachague viongozi makini watakaosimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM na kusimamia fedha zinazotolewa na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali katika Mitaa, Vijiji na Vitongoji.
Aidha, amewataka Viongozi watakaochaguliwa wawatumikie wananchi ipasavyo, watoe huduma bora na kusimamia maelekezo ya Serikali ikiwemo kampeni ya Nishati Safi ya kupikia ambapo kwa kuanza Serikali imefunga jiko la kisasa la kupikia katika shule mpya ya Sekondari ya Wasichana Namtumbo.
"Nendeni mkaishi kwenye shida za Wananchi na kuwapatia nafasi, muwasikilize na mtatue changamoto zao, na ombeni kura kistaarabu kwa kuwa mema mengi ameyafanya Rais na kila mtu anaona, wala hayahitaji tochi." Amesisitiza Mhe. Kapinga
No comments:
Post a Comment