Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo (Mb.), ameshiriki Mkutano wa Mawaziri na Viongozi wa Juu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) uliofanyika leo tarehe 21 Novemba, 2024 katika Hotel Hyat Regency jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wenye lengo la kujadili utekelezaji wa afya kwa wote na namna ya kukabiliana na dharura nchini ulihudhuriwa na Mawaziri mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na umeongozwa na Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pamoja na mambo mengine, majadiliano ya mkutano huo yatawezesha kubaini mapungufu na uwezo wa nchi kukabiliana na dharura za kiafya na majanga mbalimbali na kufanya hamasa kwa viongozi kuwezesha upatikanaji wa rasilimali na mbinu bora za utekelezaji wa afya kwa wote.
Aidha, Waziri mkuu amewasilisha shukrani za Serikali ya Tanzania kwa Washirika na Wadau mbalimbali wa maendeleo wanaoshirikiana na Serikali katika kutatua changamoto katika Sekta ya Afya na Majanga mbalimbali yanayoikumba nchi kwa nyakati tofauti.
Hivyo ameeleza azma ya Serikali ni kuendelea kushirikiana na wadau kutoka ndani na nje ya nchi katika kupambaba na majanga na kuongeza uwezi wa serikali kujiandaa katika dharura.
No comments:
Post a Comment