October 04, 2024

WIZARA YA MADINI, TUME YA MADINI NA BOT YAKUTANA NA WADAU WA MADINI

Na Mwandishi wetu, Dodoma
Ikiwa ni mkakati wa kujenga uelewa kwa wadau wa madini kuhusu utekelezaji wa kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini Sura 123, leo Oktoba 04, 2024 Wizara ya Madini imeratibu mkutano wa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini uliofanyika jijini Dodoma ambapo elimu kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo imetolewa na wataalam kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
 
Viongozi walioshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Kamishna Msaidizi – Uendelezaji Migodi, Mhandisi Ally Samaje aliyemwakilisha Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, Meneja wa Masoko ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Lameck Kakulu, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini, CPA. Venance Kasiki na watendaji wengine kutoka Tume ya Madini.
 
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Kamishna Msaidizi – Uendelezaji Migodi kutoka Wizara ya Madini, Mhandisi Ally Samaje amesema kuwa lengo la maboresho ya sheria hiyo inayomtaka kila mchimbaji na mfanyabiashara wa madini kutenga angalau asilimia 20 ya dhahabu inayozalishwa kwa ajili ya kuisafisha hapa nchini na kuiuzia BoT kabla ya kuisafirisha nje ya nchi ni kuimarisha uchumi wa nchi na kuongeza akiba (reserve) ya dhahabu nchini.
 
Ameendelea kusema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini wanafanya kazi katika mazingira mazuri pasipo kuathiri biashara zao.
 
Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo ameongeza kuwa sababu nyingine ya maboresho ya sheria hiyo ni kuhamasisha mnyororo wa shughuli za madini kufanyika nchini kuanzia kwenye uchimbaji, uchenjuaji, usafishaji na biashara ya madini.
 
Wakati huohuo, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina sambamba na kuipongeza Serikali kwa maboresho ya Sheria za Madini ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kuendelea kuangalia namna bora ya kuwawezesha watanzania kushiriki katika Sekta ya Madini na kuendelea kutatua changamoto  wanazokabiliana nazo wadau wa madini.








No comments:

Post a Comment