MHANDISI Assa Mwakilembe kutoka Tume ya Madini Sehemu ya Maabara, amewahimiza wadau katika Sekta ya Madini kuhakikisha wanatumia maabara ya Tume ili kuwa na uhakika kwenye kazi yao ya uchimbaji.
Amesema kuwa, maabara hiyo ni eneo litakaloweza kuwasaidia na kujua wingi na ubora wa madini waliyozalisha au wanayotarajia kuzalisha ambapo pia itasaidia kupata thamani halisi wakati wa mauzo.
Mhandisi Mwakilembe ameyasema hayo leo Oktoba 11, 2024 kwenye Maonesho ya Saba ya Kimataifa ya Madini yanayofanyika mkoani Geita katika viwanja vya EPZA Bombambili ambapo Tume ya Madini inashiriki kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo sahihi katika Sekta ya Madini na kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta hiyo.
“Tume ya Madini inayo maabara ya kisasa pale Msasani jijini Dar es salaam ambayo inahusika na uchunguzi na upimaji wa ubora wa sampuli za madini kama mikuo ya dhahabu (bullion), makinikia ya shaba (copper concentrate), Madini ya kinywe (graphite) kwa kutumia teknolojia adimu na bora ya kuchoma sampuli katika moto (fire assay method),”amesema Mwakilembe.
Aidha, amesema kuwa jukumu la Maabara ya Tume ya Madini ni kuhakikisha wadau wanajua ubora na wingi wa madini wanayozalisha na kuuza, hivyo, maabara ipo katika maonesho haya kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha wadau wanapata huduma bora ya upimaji sampuli pia kutoa ushauri wa kitaalam.
Amesema kuwa, mbali na maabara hiyo pia majukumu mengine ya Tume ni Kuratibu uendelezaji wa Sekta ya Madini kwa Kutoa leseni za Utafiti na uchimbaji wa madini, kuratibu fursa zitokanazo na uwepo wa Sekta ya Madini na kuhamasisha ushiriki wa Watanzania kwenye mnyororo wa Sekta ya Madini.
“ Aidha, Tume ina jukumu la kusimamia na kuhakikisha mazingira yanalindwa na wachimbaji. Pia usalama wa maeneo ya kazi na wafanyakazi wa migodini ikiwa ni pamoja na udhibiti wa uzalishaji wa taka sumu, uhifadhi wake na mipangilio ya taka hizo kwa kufuata viwango “standards” vinavyokubalika,” amesisitiza Mhandisi Mwakilembe.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Hexad, ambayo inajihusisha na uchimbaji na utafiti wa madini iliyopo Mgasa mkoani Geita, Fortunatus Luhemeja amesema kwa sasa wachimbaji wadogo wamekuwa na mwamko wa kutumia teknolojia ya kisasa na kuishauri Tume ya Madini kufunga Maabara - Kanda ya Ziwa ili iwe rahisi kutoa huduma kwa urahisi na haraka kwa wachimbaji.
Amesema kuwa, majibu ya sampuli yanapaswa kutolewa kwa haraka, mchimbaji anayetaka kujua uchimbaji unakwendaje ni lazima apeleke sampuli na kupata majibu siku hiyo hiyo badala ya baada ya siku tatu au nne.
“Kazi zetu kila siku lazima tufanye na Tume ya Madini, hivyo ikija huku itaturahisishia sana hasa teknolojia ya kuchoma sampuli katika moto (fire assay method), huku hakuna hiyo tunatumia ‘Acid digestion method’ hivyo ‘fire assay method’ ikija wachimbaji wengi watakimbilia na itapata soko,”amesema.
Wakati huo huo Luhemeja amesema kwenye uchimbaji ni lazima wafuate taratibu, kanuni na sheria ambazo Tume ya Madini imewaelekeza kufanya.
“Hatuwezi kusema tunafanya vizuri kama Tume ya Madini haifanyi vizuri, tunavyofanya vizuri kwenye uchimbaji wetu wa madini ya dhahabu ni kwamba kuna usimamizi mzuri sana wa Tume ya Madini na kuna miongozo inayotolewa ya mara kwa mara,”amesema Luhemeja na kuongeza,
“Utatuzi wa haraka wa migogoro unaofanywa na Tume ni jambo la kufurahisha, ni kama Tume imejiapiza kutokuwa na migogoro kwenye Sekta ya Madini hasa kwenye uchimbaji, kuhakikisha Sekta inakua kwa kasi bila vikwazo, Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa mfano hapa Geita imekuwa ikifanya kazi kwa karibu sana na sisi wachimbaji kuhakikisha tunafanya kazi katika mazingira mazuri na kutatua migogoro kwa haki.
No comments:
Post a Comment