October 25, 2024

MFUKO WA SELF WAELEZA MAFANIKIO TANGU KUANZISHWA KWAKE

Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda akipokea zawadi kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF Microfinance Fund (SELF MF), Santiel Yona wakati alipotembelea katika banda la taasisi hiyo katika maadhimisho ya wiki ya Huduma za Fedha  inayofanyika Mbeya Leo Oktoba 25, 2024.
*********
Mfuko wa SELF umebainisha mafanikio yake tangu kuanza kazi mwaka 2014, ambapo umefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 303 na kuwafikia walengwa 296,000.

Akizungumza leo Oktoba 25, 2024, katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayofanyika viwanja vya Luanda Nzovwe jijini Mbeya, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF Microfinance Fund (SELF MF), Santiel Yona, alisema kuwa mfuko huo ni wa Serikali na unalenga kutoa mikopo na huduma za kifedha kwa wananchi.

"Tangu 2014, tumepata mafanikio makubwa. Tumetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 303 na kuwafikia walengwa 296,000," alisema Yona.

Aliongeza kuwa kupitia uzoefu waliopata, wamejifunza kuwa utoaji wa mikopo unapaswa kuambatana na elimu ya kifedha ili kuhakikisha wakopaji wanaelewa na hatimaye kurudisha mikopo kwa urahisi.

“Katika kipindi hiki chote tumejifunza kuwa utoaji wa mikopo unapaswa kuendana na elimu ya fedha, jambo ambalo limetusaidia sana. Wakopaji wetu wanaelewa vizuri na wanaweza kurudisha mikopo,” alieleza Yona.

Aidha, alibainisha kuwa mikopo hiyo, ikitolewa pamoja na elimu ya kutosha, inaweza kusaidia kuondoa mikopo isiyo na tija kama "Kausha Damu," ambayo inakandamiza watu wanaokopa bila kufahamu namna ya kuitumia vyema.

Yona alihitimisha kwa kushukuru kwa kushiriki Wiki ya Huduma za Fedha jijini Mbeya na kuahidi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, akiamini kuwa kufanya hivyo kutachangia kubadili maisha ya Watanzania.

"Tunashukuru sana kwa kushiriki Wiki ya Fedha hapa Mbeya. Tumeweza kutoa elimu kwa wananchi wengi, na tutaendelea na jukumu hili ili kusaidia kubadili maisha ya Watanzania," alisema Yona.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda akipata maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF Microfinance Fund (SELF MF), Santiel Yona wakati alipotembelea katika banda la taasisi hiyo katika maadhimisho ya wiki ya Huduma za Fedha  inayofanyika Mbeya Leo Oktoba 25, 2024.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda akisaini kitabu cha wageni  wakati alipotembelea katika banda la  SELF Microfinance Fund kwenye maadhimisho ya wiki ya Huduma za Fedha  inayofanyika Mbeya Leo Oktoba 25, 2024. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF Microfinance Fund (SELF MF), Santiel Yona.
Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment