Kamati ya tiba na Afya ya Shirikisho la Michezo ya Wizara,Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), imezielekeza timu shiriki kwenye michezo hiyo kuanzia mwakani zinahakikisha zinamjumuisha daktari katika kikosi chao ili kufanikisha masuala ya tiba katika kituo cha michezo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Matibabu na Tiba ya SHIMIWI, Dkt. Victor Ngotta, ambaye amesema kumekuwa na changamoto ya uhaba wa madaktari wa kutoa huduma kulingana na wingi wa timu shiriki.
Dkt. Ngotta amesema michezo inakadiriwa kushirikisha watumishi wa umma zaidi ya 2000 ambao wanakuwa wakicheza michaezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, netiboli, kuvuta kamba, kuendesha baiskeli, riadha, bao, karata, draft na darts.
“Tumekuwa na upungufu wa madaktari na wachezaji ni wengi tumekuwa na michezo yetu ya siku zote ambayo inatumia nguvu, na wachezaji wamekuwa wakipata majeraha ya viungo vya mwili, inatulazimu kama kamati kuchukua madaktari waliokuja na timu na kwenda kuwahudumia wachezaji wa timu ambazo hazina madaktrari endapo wanakuwa wamepata majeraha,” amesema Dkt. Ngotta.
Amesema baadhi ya majeruhi wametibiwa uwanjani na kuendelea na matibabu kwenye kambi zao, lakini wapo nane baadhi wakiwa wamevunjika mguu, na wameweza kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya mkoa wa Morogoro, kwa ajili ya uchunguzi zaidi kutokana, lakini kati yao mmoja aliyevunjika mfupa wa bega alipewa rufaa kwenda hospitali ya KCMC Moshi.
Hatahivyo, amesema wachezaji wamekuwa wakifuata maelekezo kutoka kwenye timu yake ya tiba na afya, hususan ya kuzingatia milo wanayokula, kunywa maji kwa wingi na kupata muda wa mapumziko ili kuuweka mwili sawa, maana mwili umepata mabadiliko kutokana na baadhi yao kutokuwa na mazoea na muda wa kufanya mazoezi ya viungo.
Pia Dkt. Ngotta amesema kuwa wamekuwa na desturi ya kutoa elimu kwa viongozi wa timu shiriki ili iwe rahisi wao kuhudumia wachezaji wao endapo watakuwa hawajaja na daktari.
No comments:
Post a Comment