October 11, 2024

BALOZI NCHIMBI ATOA UELEKEO CHAGUZI ZIJAZO


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Balozi Emmanuel Nchimbi, akizungumza na viongozi pamoja na wanachama wa CCM wilaya ya Kahama, leo Oktoba 10 2024 akiendelea na ziara ya kuimarisha chama na kuhamasisha wananchi kuhusu kujiandikisha katika daftari la mpiga kura mkoa  wa Shinyanga. (Picha na CCM )
*************
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amewataka viongozi wa CCM kutenda haki kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Novemba mwaka huu.


Akizungumza na viongozi na wanachama mbalimbali wa CCM Wilaya ya Kahama leo, tarehe 10 Oktoba 2024, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Shinyanga, akiambatana na Katibu wa NEC - Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Amos Gabriel Makalla, na Katibu wa NEC - Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ndugu Rabia Hamid Abdalla.

Balozi Nchimbi amesema kila mwanachama wa CCM ana haki sawa na mwingine, akisisitiza kuwa ni kinyume cha maadili ya CCM kumnyima mtu mwenye sifa bora nafasi ya uongozi kutokana na chuki binafsi.

“Tunakoelekea kwenye chaguzi zetu, utekelezaji wa haki unatakiwa. Acheni kupanga safu. Viongozi bora ndio wapitishwe. Ni kosa kubwa la kimaadili ndani ya CCM kiongozi kumkamia mwanachama… kwamba eti safari hii nitahakikisha fulani anakatwa kwenye chama chetu. Hiyo hapana, kwani kila mwanachama ndani ya CCM ana haki sawa na mwingine.”

“Tuna watu, ukimalizika tu uchaguzi ndani ya Chama chetu, anaanza upelelezi nani ambae hajamuunga mkono na kuanza kumshughulikia. Hiyo ni tabia mbaya na haikubaliki. Kwani mtu kukupigia kura ni haki yake, akikunyima kura ni haki yake pia. Kuna wengine viongozi wamejigeuza kuwa miungu watu. Hiyo hapana. Viongozi wazuri husambaza upendo,” amesema Balozi Nchimbi.

Katibu wa Idara ya Itikadi, Uenezi, na Mafunzo ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Amos Makalla, ametoa wito kwa Watanzania na wanachama wa CCM kujiandikisha katika daftari la makazi ili kuhakikisha wanapata fursa ya kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Katika hotuba yake, Makalla alisisitiza kuwa zoezi hili ni muhimu kwa kila mwananchi anayependa kushiriki katika kuchagua viongozi watakaoleta maendeleo ya haraka katika maeneo yao.

Aidha, Makalla aliwataka mabalozi wa CCM kote nchini kushirikiana na wananchi kwa kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, akieleza kuwa hatua hiyo itawawezesha kuchagua viongozi bora kutoka ndani ya chama.

Aliongeza kuwa ni jukumu la mabalozi kuhakikisha wanachama wa chama tawala wanashiriki kikamilifu ili kuhakikisha utekelezaji wa sera za chama kwa mafanikio makubwa.

Katibu huyo pia alieleza kuwa ili maendeleo yafikiwe kwa haraka, ni muhimu kuchagua viongozi wenye weledi na maono ya maendeleo, akiongeza kuwa chama kinaendelea kutoa mafunzo kwa viongozi wake ili kuwaandaa vyema kwa majukumu hayo.

Alisema kuwa kuchagua viongozi sahihi ni hatua ya msingi katika kujenga jamii yenye maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Katibu wa Idara ya Siasa na Mambo ya Nje wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Rabia Abdalla, alisisitiza umuhimu wa mshikamano na upendo miongoni mwa viongozi na wanachama wa CCM.

Alieleza kuwa kuwa na uhusiano mzuri kati ya viongozi kunaimarisha utekelezaji wa majukumu yao na kuleta matokeo bora kwa wananchi.

Rabia aliongeza kuwa viongozi wanapaswa kuwa mfano mzuri wa kuigwa katika kuonyesha upendo, umoja, na mshikamano, akisema kuwa hayo ni maadili muhimu kwa kiongozi yeyote anayejali maslahi ya wananchi.

Alisisitiza kuwa chama kitatilia mkazo maadili hayo katika kuhakikisha kuwa viongozi wake wanatimiza wajibu wao kwa ufanisi.

Katika hitimisho, viongozi wote walikubaliana kuwa ni jukumu la kila mwanachama wa CCM kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi huo kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment