September 15, 2024

WATENDAJI WATAKIWA KUWA MAKINI UBORESHAJI WA DAFTARI











Na. Mwandishi Wetu

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewaasa watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura kutekeleza majukumu yao kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji.
 
Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari ngazi  ya mkoa na halmashauri za mkoa wa Dodoma leo tarehe 14 Septemba, 2024.
 
“Vifaa hivi (vya uboreshaji wa Daftari) vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na vinatarajiwa kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini. Kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu.,” amesema Jaji. Mbarouk wakati akisisitiza umuhimu wa kutunza vifaa hivyo.
 
Amewaasa watendaji hao kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili waweze kuyafanyia kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza.
 
Wakati huohuo, akifungua mafunzo kama hayo mkoani Singida, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Dkt. Zakia Mohamed Abubakar amesema matokeo bora ya zoezi la uboreshaji wa Daftari yatatokana na Matokeo bora ya zoezi hili yanategemea uwepo wa ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji, serikali, vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi.
 
“Ninawasihi muwe na ushirikiano mzuri na wa karibu na Tume wakati wote mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu na ikiwa mnahitaji ufafanuzi au maelekezo yeyote, msisite kuwasiliana na Tume,” amesema mjumbe huyo wa Tume.
 
Mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya Mzunguko wa tano wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao utajumuisha mkoa wa Dodoma katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Halmashauri za Wilaya ya Bahi, Chamwino na Kongwa, mkoa wa Manyara katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu na Wilaya ya Kiteto na Simanjoro na mkoa wa Singida.
 
Uboreshaji wa daftari kwenye maeneo hayo utaanza tarehe 25 Septemba, 2024 hadi tarehe 01 Oktoba, 2024 na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.

No comments:

Post a Comment