Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Baadhi ya viongozi wa timu zinazoshiriki kwenye mashindano ya 38 ya Shirikishpo la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) wamepongeza uendeshaji wa michezo hiyo inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali mkoani Morogoro.
Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Mahakama Tanzania, Fidelis Choka amesema maandalizi hadi kuanza kwa michezo hiyo kumefanyika vizuri, lakini ametoa angalizo la suala la wachezaji wasiowaajiriwa wa taasisi, wizara na ofisi za wakuu wa mikoa kushiriki kwenye michezo hii kinyume na taratibu.
Choka ametoa wito wa kutafutwa kwa mwarubaini wa tatizo hili ili kuliondoa kabisa na kubaki na wanaostahili, ili kuleta ushindani na baadaye washiriki wakaongeze bidii na tija mahala pa kazi.
“Nadhani utafutwe mfumo ambao utaondoa hili doa ambalo sasa linaendelea kuota mizizi kila uchao,” amesisitiza Choka.
Naye Katibu Mkuu wa Klabu ya Michezo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Amie Lupondo ameomba watawala kuruhusu timu zao kushiriki kwenye michezo hii pia kuwanunulia vifaa, kuwapa posho kwa wakati na kuwatembelea kwenye kituo cha michezo kwani inaongeza hamasa.
Kwa upande wake Kiongozi wa tiu ya Ofisi ya Rais Ikulu, Said Akubemba amelitaka shirikisho kushirikiana na mkoa husika kutangaza michezo hii ili wananchi waweze kufika kwa wingi kupata burudani kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Naye Kocha Msaidizi wa timu ya Kuvuta kamba ya Wizara ya Uchukuzi, Nicas Luanda amesema mashindano ya mwaka huu 2024 yamekuwa na ushindani mkubwa ambao ameshughudia ongezeko la timu za mchezo huo ambazo zinaleta burudani uwanjani, lakini ameomba washiriki wengine wale ambao hawana mchezo huo katika klabu zao kuuongeza.
Lakini, Luanda ameiomba kuwe na utaratibu wa timu kubwa kuwa ndio vinara kwenye makundi ya hatua za awali na ti,u nyingine ndogo ziwe chini yao, itaongeza ushindani na kuongeza morali.
Kwa upande wake mjumbe wa klabu ya michezo ya Maji, Grace Lazaro amepongeza shirikisho kwa jitihada zake za uhamasishaji michezo mahala pa kazi na sasa mashindano yanashirikisha timu nyingi.
No comments:
Post a Comment