September 28, 2024

NAIBU WAZIRI MAMBO YA NJE AWAFUNDA WASHIRIKI WA SHIMIWI










Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Washiriki wa michuano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), amewaasa washiriki kucheza michuano hiyo kwa upendo, undugu na amani kwa kuwa inasaidia kuondoa msongo wa mawazo mahala pa kazi na majumbani.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 27 Septemba, 2024, na Naibu Waziri wa Mambo ya nje na Ushirkiano wa Kimataifa (anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki), Dennis Londo wakati alipozungumza na baadhi ya timu za mchezo wa netiboli zilizokuwa zikicheza hatua ya 16 bora ikiwemo timu ya wizara yake.

Mhe. Londo amesema michezo ni nidhamu, mahusiano na urafiki na pia kufahamiana baada ya kutoka nje ya mazingira ya kazi, na kubadilishana uzoefu baina ya watumishi wa mahali fulani pa kazi na mwingine ambapo kunachangia kuongeza tija makazini.

Amesema wanaodhani michezo ni kupoteza muda wanakuwa hawajielewi, ambapo ameweka msisitizo wa kutumia msemo wa kilatini aliosema kuwa “akili safi inakaa kwenye mwili safi”, ambapo mwili dhoofu hauwezi kukaa kwenye akili safi, hibvyo amesema mazoezi ni mazuri ili kuifanya akili ifanye kazi kwa bidii.

Mhe. Londo amesema serikali inatumia gharama kubwa kwa ajili ya michezo ili watumishi waweze kuongeza tija na ushirikiano mahala pa kazi, endapo awali ushirikiano umekuwa ukilegalega kutokana na sababu moja au nyingine.

“Michezo ni undugu, michezo ni urafiki lakini pia napenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha mkoani Morogoro, huwa nawaambia wenzangu kule Bungeni kuwa wakati nikiwa shule ya msingi nimecheza sana kwenye uwanja huu wa Jamhuri na mama yangu alikuwa mchezaji nguli wa mchezo wa netiboli, hadi kachezea timu ya taifa (Innocensia Banzi) na pia alikuwa mwalimu wa michezo wa miaka mingi, name ni mwanafamilia wa michezo na bungeni nacheza basketball (mpira wa kikapu),” amesema Mhe. Londo.

No comments:

Post a Comment