September 27, 2024

BAHI WAONESHA MWITIKIO UBORESHAJI DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA







Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule, leo Septemba 26, 2024, ametembelea na kukagua baadhi ya vituo vya kuboreshea Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma ili kuona mwitikio wa wananchi katika zoezi hilo.

Mhe. Senyamule amejionea namna zoezi hilo linavyokwenda na kupewa taarifa kuwa hakuna changamoto iliyojitokeza tangu kuanza kwa zoezi hilo Septemba 25, 2024. 

Aidha ametumia nafasi hiyo kuendelea kutoa hamasa kwa wananchi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao.

“Nendeni mkajiandikishe ili mwaka kesho kila mtu mwenye sifa aweze kwenda kupiga kura. Mungu ametupa baraka, Nchi yetu ina demokrasia, kila mtu anatakiwa kupata haki ya kuchagua kiongozi anayemtaka, wajibu wetu ni kuitumia haki hiyo ili kupata viongozi tunaowataka.” Mhe. Senyamule  

Zoezi hilo lililoanza Septemba 25, linatarajiwa kutamatika Oktoba Mosi, 2024 ambapo katika  Uboreshaji huo wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utamuwezesha mwananchi mwenye sifa kupata haki yake ya msingi ya kupiga kura katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ambao utahusisha Udiwani, Ubunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kata zilizotembelewa ni Ibihwa, Mpamantwa na Bahi Sokoni ambapo zote zinaonesha mwitikio mzuri.

No comments:

Post a Comment