July 15, 2024

WIZARA YA ARDHI YATOA HATI MILIKI 1,134 SABASABA, DAR ES SALAAM





Na Eleuteri Mangi, Dar es Salaam
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetumia fursa ya Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kuandaa, kusajili na kutoa Hatimiliki kwa wamiliki wa ardhi wa mikoa ya Dar es salaam, Dodoma na Pwani.

Hati hizo huimarisha usalama wa miliki, kudhibiti na kupunguza migogoro ya ardhi, kuongezeka kwa ardhi iliyopangwa na kumilikishwa, na kutumia ardhi kama dhamana katika taasisi za fedha na vyombo vya sheria.

Ndiyo maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza viongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Mkazi kusimamia haki za watu kwenye sekta ya ardhi. 

Hii ni pamoja na utekelezaji wa mradi mkubwa wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaoendelea kutekelezwa kwa kutambua kila kipande cha ardhi, Kupanga, Kupima na Kusajili kwa kutoa Hati katika Halimashauri 67 nchini. 

“Simamieni haki za watu kwenye ardhi, ardhi ndiyo msingi wa kila kitu, ardhi ndiyo utajiri wa watu, ardhi ndiyo utajiri wa nchi, kila kitu ni ardhi” anasema Rais wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Msukumo huo wa Rais, umeifanya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutumia fursa ya maonyesho ya Sabasaba mwaka huu kuanzia Juni 28, 2024 hadi Julai 13, 2024 kutoa jumla ya hati 1,134 ambapo kwa mkoa wa Dar es salaam zimetolewa hati 981 Dodoma hati 33 na Pwani hati 120 na wananchi zaidi ya 2700 wamepata elimu na huduma mbalimbali za ardhi kwenye banda hilo.

Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es salaam 2024 yalifunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Filipe Jacinto Nyusi ambaye aliambatana na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo wakisihi wafanyabiashara kusajili bidhaa zenye ubora katika Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) na kutafuta masoko nje ya nchi.

Umuhimu huo wa hati miliki za ardhi umebainishwa na Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa wakati akiwasilisha Bungeni Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa kuainisha maeneo ya kipaumbele ya Wizara yake kwa mwaka wa Fedha 2024/25.

Vipaumbele vitano ambavyo ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi mijini na vijijini, kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, kuimarisha mifumo ya TEHAMA wa kutunzia kumbukumbu, utoaji wa huduma na upatikanaji wa taarifa za ardhi, kuhakikisha uwepo wa nyumba bora, ukuaji wa sekta ya milki na maendeleo ya makazi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuimarisha mipaka ya kimataifa.

Akizungumza na wananchi Julai 6, 2024 mara baada ya kuwahudumia kwenye banda la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa maonyesho hayo, Naibu Katibu Mkuu Lucy Kabyemera amesema wizara hiyo imeshiriki maonyesho hayo kwa lengo la kuwahudumia wananchi katika sekta ya ardhi hatua inayowasaidia katika shughuli za kibiashara na kiuchumi kwa kutoa elimu ya masuala ya ardhi.

"Wananchi wakiwa na uelewa watapata msukumbo wa kushiriki kupanga, kupima na kumilikishwa ardhi zao ili kuwa na usalama wa milki za ardhi hatua itakayowasaidia kuondokana na migogoro inayotokana na kukosekana kwa elimu ya ardhi” amesema Naibu Katibu Mkuu Kabyemera.

“Tunatoa huduma za utoaji wa hati, sasa tunatoa hati za kidijiti kwa mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma tumeanza kutoa hati hizo, kwenye maonysho haya tunatoa hati kwa mikoa ya Dar es salaam, Dodoma na Pwani” 

Naibu Katibu Mkuu Kabyemera amesisitiza kuwa Wizara hiyo pia imetumia furs ya maonyesho hayo kuendesha Kliniki ya Ardhi kwa kuwahudumia na kuwasikiliza wananchi kwa kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao.

Akionesha kuridhishwa na huduma wakati wa maonyesho ya Sabasaba, Waziri na Mbunge wa zamani wa Hanag Dkt. Mary Nagu amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa kwa kazi nzuri ya kuwahudumia Watanzania kwenye sekta ya Ardhi ambapo watu wengi wamerahisishiwa kupata hati zao na amesisitiza huduma hiyo itolewe kwa kasi hiyo hiyo kwenye ofisi zote za ardhi nchi nzima.

“Naomna Watanzania wote wapate haki hiyo ya kupata hati miliki ya ardhi zao, unapokuwa na hati unathamani kubwa ya rasilimali ardhi uliyonayo, napenda watanzania wote mpaka vijijini wawe na hati za maeneo yao ili thamani ya ardhi ijulikane na watumie rasilimali yao kukuza uchumi wao” amesema Dkt. Nagu. 

Wanamilia ya Bw. Martin Sintala na Juliana Lucas wakazi wa mtaa wa Akachube Makumbusho jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa wananchi waliopata Hati Miliki ya pamoja ya kiwanja chao wakati wa maonyesho hayo hatua inayowasaidia kila mwanafamilia kuwa na haki ya kumiliki ardhi hiyo.

Kuna faida lukuki za kuwa na hati miliki ya kiwanja chako, ni muhimu kupanga, kupima ardhi yako na umiliki kisheria kwa usalama na maendeleo ya baadae.

Unapokuwa na hati unatambuzi kisheria kuwa wewe ni mmiliki halali wa kipande hiko cha ardhi, unaongeza thamani ya ardhi, ukipanga, ukipima na ukamiliki kisheria ardhi yako inapanda thamani kwa kuwa umiliki wako unatambulika kisheria.

Faida nyingine ni kuongeza usalama katika ardhi yako, hivyo kuzuia mtu yeyote kujimilikisha au kufanya shuguli yeyote katika ardhi yako bila ridhaa yako, kutumika kwa hati miliki yako kama dhamana katika kuomba mikopo benki na taasisi za kifedha, hivyo kukuinua kiuchumi pamoja na kuondoa migogoro na majirani zako na pia usumbufu pindi unapotaka kuiuza ardhi hiyo.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi anaamini kuwa ni rasilimali kuu ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na ustawi wa watu wote na imeleta fursa kwa wananchi katika maonyesho ya Sabasaba wapate haki zao za kuwa na hati miliki ya ardhi.

Migogoro ya ardhi imebebwa katika taswira ya changamoto za umiliki wa ardhi kwenye mirathi, migogoro ya matumizi ya ardhi, mipaka ya mtu na mtu, kijiji na kijiji, wilaya na hata mikoa. 

Maonyesho ya 48 ya Bishara ya Kimataifa yamehitimishwa Julai 13, 2024 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambapo zaidi ya nchi 26 zimeshiriki maonyesho hayo.

No comments:

Post a Comment