July 24, 2024

WAZIRI MKUU APONGEZA MCHANGO WA SEKTA BINAFSI NCHINI








Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, ametoa shukurani zake kwa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa mafanikio yao katika kukuza na kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta hiyo hapa nchini.

Waziri Mkuu ameyasema hayo katika hafla ya kusherehekea Miaka 25 ya TPSF, kwenye hafla ya chakula cha jioni ya wadau iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Super Dome, Masaki, Dar es Salaam ikiwa ni kilele cha mahadhimisho ya wiki ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSW24) mwaka huu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu ameihakikishia sekta binafsi kuwa, serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inafanya kila jitihada kusaidia sekta binafsi katika kusukuma mbele ustawi wa uchumi nchini kwa kujibu hoja zao na kuondoa vikwazo vyote vinavyozuia ukuaji wa sekta hiyo. 

“Serikali yetu ni sikivu na imekuwa mstari wa mbele katika kuwasikiliza wafanyabiashara na sekta husika, tunatambua mchango mkubwa ambao TPSF imetoa kwa miaka 25 iliyopita katika kuleta mabadiliko katika sekta binafsi na kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na sekta binafsi. Napenda kuipongeza bodi ya wakurugenzi na timu ya menejimenti ya TPSF kupitia masharti yake mbalimbali ya kiuongozi kwa kushirikiana na mashirika mengine na wafanyabiashara kwa ujumla kuandaa shughuli hii chanya ya kujadili na kuweka mikakati madhubuti ya maendeleo ya taifa letu.

"Nataka niwahakikishie kuwa Serikali yetu sikivu inayoongozwa na Rais wetu Mhe Dkt.Samia Suluhu Hassan imejipanga kuboresha miundombinu ili sekta binafsi iweze kuimarika na serikali ikusanye kodi na kujenga miundombinu kwa ajili ya wananchi," aliongeza kusema Waziri Mkuu.

“Pamoja na hayo, Rais wetu anaendelea kuweka juhudi za kuboresha mazingira ya sekta binafsi kwa lengo la kuondoa mdororo wa kiuchumi kwa kila Mtanzania. Serikali pekee haiwezi kumudu Watanzania wote hivyo uboreshaji wa sekta binafsi, ni uboreshaji wa Taifa. Leo ni shuhuda kwamba, sisi kwa pamoja tunaweza kufanya kazi na kulifanya taifa hili kuwa taifa kubwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Bw. Raphael Maganga alimshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi wa hafla hiyo kwani ni muhimu kwa sekta binafsi kukaa meza moja na kubadilishana mawazo na serikali kuu sio tu kuadhimisha miaka 25 ya sekta binafsi lakini pia kuangalia ni mambo gani makubwa wanaweza kuyafanya kwa pamoja ili kuboresha sekta binafsi nchini kwa ujumla.

“Kwa niaba ya Wakurugenzi wenzangu wa Sekta Binafsi nchini, tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dk. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ya awamu sita kwa kutuwekea mazingira rafiki na kuweka milango wazi kwa mijadala mbalimbali ya kuboresha sekta yetu,” alisema Maganga.

"Pia tunapenda kushukuru na kutambua michango na msaada kutoka kwa washirika wengine wa maendeleo ikiwa ni pamoja na misaada kutoka nje kupitia Mabalozi na Jumuiya za Wafadhili wa Kigeni ambao wamefanya kazi nasi bila kuchoka kuhakikisha tunasaidia na kukuza sekta binafsi." Maganga aliongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPSF, Bibi Angelina Ngalula, aliishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara na sekta binafsi kwa ujumla ili kuweza kutekeleza majukumu yao.

"Sisi tusingekuwa hapa leo, kama Serikali isingetupa ushirikiano iiliyotupa kwa kipindi cha miaka 25. Pia niwashukuru watangulizi wangu, wenyeviti wa zamani wa bodi kwa kuubeba mwenge huu kwa zaidi ya miongo miwili. Sekta binafsi itaendelea kufanya kazi na Serikali na kushirikiana wakati wote lengo ni kuona mambo yanakwenda vizuri na kila upande unanufaika.

Aidha, aliongeza kuwa, “Mchango wa sekta binafsi katika uchumi ni mkubwa na TPSF ina mchango mkubwa katika kutoa utetezi kwa niaba ya sekta binafsi na kuunda chombo kikuu cha taasisi nyingine zote zinazofanana. Matokeo ya hili yameonekana, kumekuwa na makampuni mengi yanayowekeza na kustawi hapa nchini na kutengeneza nafasi nyingi za kazi, bidhaa na huduma zinapatikana na ustawi wa kiuchumi kupatikana katika ngazi ya mtu binafsi na kitaifa”. 

“Hii si kusema, tumefika. Bado tuna safari ndefu ya kuleta ukuaji wa kisekta, hata hivyo njia tunayopita, tunaamini ni njia sahihi”. Aliongeza. 

Hafla hiyo ya kuadhimisha miaka 25 ilihudhuriwa pia na wadau mbalimbali wakiwemo Wakurugenzi Wakuu wa Kampuni, Maafisa Waandamizi wa serikali, wawakilishi kutoka mashirika mengine ya sekta ya binafsi, Wanadiplomasia na mashirika ya Misaada ya kigeni.

No comments:

Post a Comment