July 26, 2024

VILABU VINAVYOSHIRIKI MICHEZO YA MEI MOSI WAHIMIZWA KULIPA ADA YA USHIRIKI KWA WAKATI







Na Mwandishi Wetu
TAASISI na Mashirika ambayo yana malimbikizo ya ada za ushiriki wa michezo ya wafanyakazi zimeombwa kulipia ada ya ushiriki mapema ili kufanikisha michezo hiyo inayofanyika kila mwaka wakati wa Siku Kuu ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi Taifa Roselyne Mathew Massam kwenye kikao cha Viongozi Vilabu vya michezo ambvyo vipo kwenye Mashirikisho ya Michezo nchini ambao wamekutana kufanya tathimini ya michezo hiyo iliyofanyika mwezi Aprili mwaka huu Jijini Arusha.

Massam, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma (SHIMUTA), amesema kuwa ucheleweshaji wa ulipaji wa ada unakwamisha ufanisi wa michezo hiyo na kusababisha kushindwa kugharimia gharama za michezo hiyo ikiwemo kulipia viwanja vizuri vyenye ubora.

Massam amesema Kamati hiyo ya Michezo ya Mei Mosi inaundwa na mashirikisho ya SHIMIWI,  SHIMUTA, SHIMISEMITA na BAMATA ambapo  katika tathimini hiyo kamati hiyo imeweka mkakati wa kuongeza timu zitakazozoshiriki mashindano  hayo mwakani ambapo mwaka huu Jumla ya timu 56 zimeshiriki ukilinganisha na timu 33 zilizoshiriki mwaka jana 2023.

Amesema kuwa Kamati imekuwa na utaratibu wa kufanya tathimini  ili kutambua changamoto zilizojitokeza zisijirudie tena hivyo kuboresha michezo ijayo iwe mizuri zaidi .

Massam, amesema kamati hiyo inaendelea kuhamasisha Wizara, Idara, taasisi, mashirika ya umaa na sekta binafsi  kuhakikisha kila mfanyakazi anafanya mazoezi na kushiriki michezo hiyo kwa ajili ya kuimarisha afya.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Michezo Taifa Alex Faustini Temba, ameishukuru Serikali kwa kutoa kibali kwa wafanyakazi kushiriki michezo hiyo ambapo mbali na kucheza michezo hiyo tofauti tofauti walichanga fedha shilingi milioni 13, ambazo walizitoa kwa Vituo vya wahutaji jijini Arusha.

Naye Mwenyekiti wa Michezo Shirika la Viwango Nchini (TBS), Nyabuchwenza Methusela, amesema michezo ya mwaka huu ilikuwa na mafanikio licha ya changamoto iliyojitokeza  ya uchelewaji wa washiriki kuhudhuria na hivyo kuathiri ratiba na kusababisha michezo kuchezwa mfululizo asubuhi na jioni.

No comments:

Post a Comment