July 08, 2024

SIJARIDHISHWA NA UJENZI WA SHULE HII – MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama dawati wakati alipokagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Lugalo wilayani Kilolo mkoa wa Iringa, Julai 8, 2024.  Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba na  wa tatu kulia ni Mhandisi wa wilaya ya Kilolo Emmanuel Sagachuma ambaye alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi  wa tuhuma za ubadhirifu.
Moja kati ya madawati yenye nyufa ambayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliagiza kuwa aliyeyatengeneza ayachukue kwa gharama zake na atengeneze mengine yenye viwago na kuyarejesha katika Shule ya Secondairi ya Wasichana Lugalo wilayani Kilolo. Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa Shule hiyo akiwa katika ziara ya mkoa wa Iringa, Julai 8, 2024.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Lugalo wilayani Kilolo mkoani Iringa, Julai 8, 2024. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipita kwenye  bweni wakati alipokagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasicha Lugalo wilayani Kilolo Mkoa wa Iringa, Julai 8, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  akionesha dirisha lisilokuwa na wavu  katika jengo la utawala la  Shule ya Sekondari ya Wasichana Lugalo wilayani Kilolo Julai 8, 2024.  Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba na wa pili kushoto ni Mhandisi wa wilaya ya Kilolo, Emmanuel  Sagachuma ambaye alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi  wa tuhuma za ubadhirifu
************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya mkoa wa Iringa na kuagiza Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Emmanuel Sigachuma asimamishwe kazi mara moja.
 
Pia ameagiza Afisa Elimu ngazi ya Sekondari ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Nelson Milanzi apewe onyo kwa kushindwa kusimamia matumizi ya fedha za ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Lugalo iliyoko kata ya Mbigili, wilayani Kilolo.
 
Pia ameagiza Mkurugenzi Mtendaji Mstaafu, Lain Ephraim Kamendu aitwe ili ahojiwe pamoja na wenzakekuhusu matumizi mabaya ya fedha hizo. Yeye alistaafu Aprili, mwaka huu na ujanzi ulianza yangu Agosti, 2023. 
 
Amefikia uamuzi huo leo (Jumatatu, Julai 8, 2024) baada ya kukagua ujenzi wa sekondari hiyo na kukuta kasoro nyingi kwenye madawati, vyumba vya maabara na bwalo la wanafunzi ilhali walishapewa sh. bilioni tatu za kukamilisha majengo yote ya shule hiyo. 
 
Kasoro kubwa zilizobainika ni ukosefu wa nyavu za kuzuia mbu kwenye baadhi ya madirisha wakati mkandarasi ameshalipwa fedha yote, viti na meza za wanafunzi kupasuka wakati havijaanza kutumika. Viti hivyo vilikabidhiwa tangu Desemba, 2023 na muda wa matazamio ulikuwa ni miezi sita lakini mkandarasi keshalipwa fedha zote.
 
Katika ukaguzi wa bwalo, Waziri Mkuu alielezwa na Mhandisi Sagachuma kwamba bwalo hilo lilitengewa sh. milioni 774 na wamekwishatumia sh. milioni 341 hadi kufikia hatua ya linta ambayo alidai ni sawa na asilimia 40 ya ujenzi wake.
 
Alipoulizwa fedha zilizobakia ziko wapi, Mhandisi huyo alijibu kwamba hazipo. Afisa Elimu Sekondari naye hakuweza kueleza ziko wapi au kama kuna vifaa vilivyokwishanunuliwa vimewekwa wapi.
 
"Unasema utajenga kwa chuma hapa juu, hizo nondo ziko wapi? Mabati yako wapi? Majiko yako wapi? Hapa tunatarajia kuwa na watoto 172, je watakula wapi hawa na masomo yameshaanza?" alihoji Waziri Mkuu bila kupatiwa majibu. 
 
“Wewe ni Afisa Elimu na kazi yako ni kusimamia ujenzi wa shule zote, ni kwa nini hukutoa taarifa ya kusuasua kwa ujenzi kwenye Kamati ya Ulinzi ya Wilaya yako? Taarifa nilizonazo ni kwamba Mkurugenzi aliyekuwepo alikuwa anakupangia kazi kwenye vituo vya mbali ili usije hapa, lakini bado ulikuwa na wajibu wa kutoa taarifa juu ya mwenendo huo.”
 
Kwenye ujenzi wa maabara za shule hiyo, Waziri Mkuu amehoji ni kwa nini mifereji ya kupitisha gesi na maji machafu imezibwa yote. “Mifereji haina vishikio, wamejaza matofali hata mwalimu akitaka kukagua mifumo ya gesi au mifereji ya maji machafu hawezi kuinua hilo tofali. Mifuniko ya mifereji inayopitisha maji, bomba za umeme na gesi kwenye maabara ya shule hiyo itolewe na irekebishwe upya,” ameagiza.
 
Amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Joachim Nyingo asimamie zoezi la kurudisha madawati yaliyoletwa ambayo ni mabovu kwa gharama za mkandarasi ili yaletwe mengine mapya. Madawati (meza na viti vyake) mengi yalikuwa yamepasuka katikati au pembeni na yalikuwa yamepangwa darasani.
 
“Nimeagiza fundi aliyejenga madirisha atafutwe, aletwe ili aweke nyavu kwenye jengo la utawala. Aliyetengeneza madawati aitwe akayatengeneze upya madawati hayo kwa viwango vinavyotakiwa na kwa gharama zake.”
 
Pia amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU, Mkoa wa Iringa, awahoji watumishi hao na aanze uchunguzi mara moja.
 
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekabidhi hati ya kiwanja chenye ukubwa wa ekari 50 kwa uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ili waweze kuanza ujenzi wa tawi la chuo hicho katika wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.

No comments:

Post a Comment