July 09, 2024

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AWAKA KISA HALMASHAURI KUTOTENGA FEDHA ZA KUKABILIANA NA MALARIA.






Baadhi ya Halmashauri za mkoa wa Singida ikiwemo IRAMBA zimeshindwa kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan linalotaka kila Halmashauri kutenga bajeti maalum kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa malaria ikiwemo ununuzi wa dawa za kupulizia mazalia ya mbu kwenye maeneo hatarishi.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Godrey Mnzava amebaini tatizo hilo akiwa katika mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Iramba wakati anakagua afua za lishe wilayani huyo na kuonyesha kutorishishwa na kasi ya baadhi ya Halmashauri katika kukabiliana na ugonjwa malaria.

Mnzava amesema agizo la Rais Samia Suluhu Hassan ni lazima litekelezwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 ugonjwa huo wa malaria uwe umetokomezwa kabisa hapa nchini.

"Tengeni bajeti kwa kutumia mapato ya ndani kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa malaria kwa sababu bado unaathiri nguvu kazi ya Taifa," amesisitiza Mnzava.

Ametoa mfano kwa Halmashauri ya Iramba ambayo inakusanya zaidi ya bilioni Mbili kwa mwaka kutoka kwenye vyanzo vyake vya mapato lakini imeshindwa kutenga shilingi milioni Saba kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa malaria jambo ambalo amesema sio zuri na halifurahishi hata kidogo.

Kuhusu matumizi ya dawa za kulevya, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuimarisha misako ambayo itasaidia kuwakamata watumiaji na wafanyabiashara za dawa hizo ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Amesema tatizo hilo lisipokomeshwa litaendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa hivyo ni muhimu kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya uzambaji na utumiaji wa dawa za kulevya ikiwemo kuwabaini watu kwa siri watu wanaofanya biashara ili waweze kukamatwa na kuwajibishwa.

Baadhi ya Viongozi wa wilaya ya Iramba wamemwahidi Kiongozi huyo wa mbio za mwenge kuwa watatekeleza maagizo yake aliyoyatoa kwa ajili ya ustawi wa wananchi wa wilaya ya Iramba na mkoa wa Singida kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment