Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa ikiwa ni utekelezaji wa Vision ya 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri, Wizara ya Madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imefanikiwa kufanya tafiti za kina za majaribio katika mikoa ya Dodoma, Geita na eneo la Kahama lengo likiwa ni mkakati wa kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 maeneo yote nchini yanafanyiwa utafiti na kuongeza kasi ya uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini.
Waziri Mavunde amesema hayo leo Januari 06, 2024 jijini Mwanza kwenye kikao chake na Menejimenti ya Tume ya Madini iliyohusisha Makamishna wa Tume ya Madini, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, Wakurugenzi, Mameneja, Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa na kuhudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali na Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga.
Amesema kuwa, tafiti za kina za majaribio zimeonesha matokeo mazuri sana na kuongeza kuwa katika awamu ya pili Wizara inapanga kufanya tafiti za kina katika mikoa ya kimadini ya Lindi, Mtwara na Mirerani lengo likiwa ni kuhakikisha taarifa za uhakika za madini yaliyopo zinapatikana na kutumika kuvutia wawekezaji katika uchimbaji wa madini yanayopatikana katika mikoa husika.
“Ninaamini kabisa hatua ya kufanya tafiti za kina hasa katika eneo la Mirerani lililopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara litaondoa tatizo la mitobozano kwenye uchimbaji wa madini ya tanzanite, maana kila kitu kitakuwa wazi,” amesisitiza Waziri Mavunde.
Ameendelea kueleza kuwa Wizara ya Madini inatarajia kufanya tafiti za kina za madini nchi nzima zitakazoondoa uchimbaji wa madini wa kubahatisha na kuongeza uwekezaji katika Sekta ya Madini ikiwemo idadi ya kampuni kubwa za uchimbaji wa madini zitakazopelekea ongezeko la watoa huduma kwenye migodi ya madini, ushiriki wa watanzania na Sekta Binafsi.
Wakati huo huo, Waziri Mavunde amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuongeza kasi ya usimamizi wa Sekta ya Madini hasa kwenye eneo la ukusanyaji wa maduhuli kwa kuhakikisha lengo linavukwa la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 882 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024.
“Mpaka Januari 05, 2024 kiasi cha shilingi bilioni 384 zimeshakusanywa, nguvu kubwa ielekezwe kwenye ukusanyaji wa maduhuli hatimaye lengo linafikiwa ifikapo mwezi Juni mwaka huu,” amesisitiza Waziri Mavunde.
Katika hatua nyingine, amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama kwenye udhibiti wa utoroshaji wa madini.
Aidha, amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuwa mstari wa mbele kuwasaidia wachimbaji wa madini kwenye shughuli zao na kuwa mstari wa mbele kwenye utatuzi wa changamoto badala ya kusubiri zifike Wizarani.
Sambamba na kuwataka maafisa madini wakazi wa mikoa kufanya kazi kidigitali na ubunifu wa hali ya juu, Waziri Mavunde amewataka kufanya kazi kwa kufuata sheria na kanuni kwenye utoaji na ufutaji wa leseni za madini ili kupunguza malalamiko.
Naye Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameongeza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto zinazowakumba wadau wa madini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miundombinu ya umeme na barabara inaboreshwa kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.
Katika hatua nyingine, Dkt Kiruswa amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuwaelekeza wawekezaji wanaopatiwa leseni za madini kuomba ridhaa kwa wananchi wa maeneo husika kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji wa madini sambamba na kuboresha huduma za jamii (CSR) na kutoa kipaumbele cha huduma na ajira kwa wakazi wa maeneo husika.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amesisitiza kuwa Wizara imejipanga kuboresha mazingira ya ofisi za maafisa madini wakazi wa mikoa ikiwemo kuongeza rasilimaliwatu pamoja na vifaa.
“Kiu yetu kubwa ni kuona shughuli za uchimbaji wa madini zinaendelea pasipo kuwepo na changamoto yoyote hivyo wananchi kuendelea kunufaika na rasilimali za madini kupitia ajira, huduma na Serikali kupata kodi mbalimbali,” amesema Mahimbali.
Awali akielezea mafanikio katika kikao hicho, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba ameeleza kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kasi ya makusanyo ya maduhuli ambayo yameendelea kuimarika kila mwaka, kupungua kwa migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na kupungua kwa matukio ya utoroshaji wa madini.
“Bado tumeendelea kuweka nguvu katika kuhakikisha miradi mikubwa ya uchimbaji wa madini inaanza mara moja ili mchango wa Sekta ya Madini kwenye uchumi wa nchi uendelee kukua,” amesema Mhandisi Samamba
No comments:
Post a Comment