January 24, 2024

WAKAZI WA VIJIJI 4O URAMBO KUNUFAIKA NA MIRADI YA MAJI SAFI

Na Lucas Raphael, Tabora
ZAIDI ya robo tatu ya wakazi Wilayani Urambo Mkoani Tabora wanatarajiwa kunufaika na miradi 2 mikubwa ya maji inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa gharama ya zaidi ya sh bil 150.

Miradi hiyo ni bwawa kubwa la maji linalojengwa na Kampuni ya Halem Construction ya Jijini Dar es salaam katika Kijiji cha Kalemela A katika kata ya Muungano kwa gharama ya sh 5.9, mradi huu utanufaisha wakazi wa vijiji 17.

Mradi mwingine ni wa Miji 28 kutoka ziwa Viktoria ambao unatekelezwa katika Wilaya 3 za Mkoa huo (Sikonge, Kaliua na Urambo) ambao unatarajiwa kugharimu zaidi ya sh bil 145 na kunufaisha wakazi wa vijiji 23 Wilayani Urambo.

Akizungumza na wakazi wa Wilaya hiyo juzi katika Kijiji cha Kalemela, Naibu Waziri wa  Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi alimshukuru Rais Samia kwa dhamira yake ya dhati ya kumaliza kero ya maji katika Wilaya hiyo na nyinginezo.

Alisema kuwa miradi hiyo ya kimkakati inayogharimu zaidi ya sh bil 150 itanufaisha wakazi wa takribani vijiji 40 kati ya 59 na vijiji 19 vilivyobakia navyo vitatengewa bajeti ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama ya bomba.

‘Wakandarasi mlioaminiwa na kupewa kazi hii fanyeni kazi yenu kwa weledi mkubwa, hakikisheni inakamilika kwa wakati kama mikataba yenu inavyoeleza kinyume na hapo tusilaumiane’, alisema.

Mahundi alifafanua kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutapunguza kwa kiasi kikubwa kero ya maji katika wilaya hiyo na dhamira ya Rais ni kumaliza kabisa tatizo la maji katika Wilaya hiyo.

Aidha aliagiza Wakurugenzi wa Mamlaka za Majisafi na Mameneja wa Wakala wa Usambazaji maji Vijijini (RUWASA) kuhakikishia huduma ya maji inafikishwa kwenye taasisi zote zilizoko katika eneo husika ikiwemo shule, zahanati, masoko na nyumba za ibada.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoani Tabora (TUWASA) Mhandisi Mayunga Kashilimu alimhakikishia Naibu Waziri kuwa watasimamia ipasavyo miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Elibariki Bajuta alimshukuru Rais Samia kwa kuwapelekea miradi hiyo ya maji na mingineyo ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Alibainisha kuwa mbali na kumwaga mabilioni hayo kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji pia katika mwaka wa fedha 2022/2023 na 2023/2024 aliwapatia zaidi ya sh bil 3.5 kwa ajili ya utekelezaji miradi 3 ya vituo vya afya.

Aliongeza kuwa vituo hivyo tayari vimeanza kazi na utaratibu unaendelea kufanyika ili kuhakikisha vinawekewa mifumo ya maji ili kuboresha usafi na suala zima la utoaji huduma.

Msimamizi wa Mradi wa Miji 28 katika Mkoa huo, Mhandisi Betty Kaduma kutoka Mamlaka ya Maji safi Shinyanga (KASHWASA) alisema kuwa mradi huo ulioanza kutekelezwa Aprili 11, 2023 unatarajiwa kukamilika Oktoba 2025.

Alibainisha kuwa jumla ya matenki 5 yatajengwa na Mkandarasi Kampuni ya Mega Engineering Infrastructures katika wilaya 3 zitakazonufaika na mradi huo yaani Sikonge, Kaliua na Urambo na jumla ya vijiji 60 vitafikishiwa huduma hiyo.

Aliongeza kuwa mradi huo utahusisha ulazaji wa mabomba makubwa na madogo yenye kipenyo cha kati ya mm 200 hadi 700 na kwenye urefu wa zaidi ya km 190 na hadi sasa mradi umefikia asilimia 32 ya utekelezaji wake.

No comments:

Post a Comment