Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel
Ndiyo, akiongea wakati akifungua mafunzo ya matumizi salama ya kemikali kwa
Wasimamizi wa Kemikali pamoja na kuelezea majukumu mbalimbali ya Mamlaka ya
Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA). Mafunzo hayo yanayofanyika kwa siku
tatu kuanzia Januari 24 hadi 26, 2024, kwenye Ukumbi wa St. Gaspar Hotel &
Conference Centre jijini Dodoma, ambapo zaidi ya wasimamizi wa kemikali 80
kutoka mikoa ya Iringa, Dodoma, Morogoro, Tabor ana Singida wanashiriki mafunzo
hayo yaliyoandaliwa na Mamlaka kupitia Ofisi ya Kanda ya Kati – Dodoma.
Mshiriki wa mafunzo, Daines Tunguhole (aliyesimama), akitoa ushauri kuhusu maboresho katika masuala ya ukaguzi wa kemikali mahala pa kazi wakati wa majadiliano kati ya wawasilisha mada na washiriki.
Meneja wa Ukaguzi wa kemikali na Maabara za Kemia, Magdalena Mtenga, akiwasilisha mada kuhusu namna bora ya kutambua, kujikinga na kemikali pamoja na kudhibiti ajali mbalimbali za kemikali.
Wasimamizi wa kemikali wakifuatilia mada
mbalimbali wakati wa mafunzo ya matumizi salama ya kemikali yanayofanyika
jijini Dodoma.
Na Okello Thomas
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), kupitia Ofisi ya
Kanda ya Kati - Dodoma imetoa mafunzo kwa wasimamizi wa kemikali kwa lengo la
kuhakikisha wanawasimamia vyema shughuli mbalimbali za kemikali katika maeneo
yao ya kazi."Matumizi ya kemikali huzalisha kemikali taka ambazo zinaweza kuleta madhara kwa afya na mazingira zisipodhibitiwa, hivyo mafunzo haya ni muhimu katika kujenga uelewa wa kujihusisha na kemikali pamoja na kuzuia ajali zinazoweza kutokea kutokana na matumizi yasiyo sahihi na salama ya kemikali,” alisema Ndiyo.
Aidha, Mkurugenzi ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo wasimamizi wa kemikali katika kujua madhara na faida ya kemikali na wote wanatakiwa kujua namna sahihi ya kutumia kemikali na kushughulikia kemikali-taka zinazozalishwa kwani ajali mbalimbali za kemikali hutokana na sababu kadhaa, zikiwemo uelewa mdogo wa sheria za nchi na ufinyu wa rasilimali watu, hivyo kuchangia matumizi ya kemikali yasiyo sahihi na udhibiti hafifu wa kemikali taka.
Naye, Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Kati – Dodoma, Gerald Meliyo, ametoa rai kwa wasimamizi wa kemikali kuhakikisha wanakuwa kwenye nafasi chanya ya kuwaelimisha wafanyakazi waliopo chini yao na pia kuwa mabalozi wa kuhamasisha wadau wengine kupata mafunzo pamoja na kueneza elimu ya matumizi salama ya kemikali katika maeneo yao ya kazi na nje ili kulinda afya za watu, wanyama na mazingira.
Kwa upande wake mshiriki wa mafunzo Mhandisi. Aron Mwaigaga, ameishauri Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kuendela kutoa elimu kwa wadau na wananchi kwa kuwaalika lakini pia kuwafikia katika maeneo yao ya kazi kwani elimu itawafikia wengi zaidi kutokana na maeneo ya kazi kuwa na wahusika wengi kwa wakati mmoja.
Mafunzo hayo ya usimamizi salama wa kemikali yanahusisha washiriki zaidi ya 80 kutoka mikoa ya Iringa, Tabora, Singida, Dodoma na Morogoro yatafanyika kwa siku tatu kuanzia Januari 24 hadi 26, 2024, jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment