December 18, 2023

WAZIRI MKUU AFUNGA MAADHIMISHO YA MIAKA 10 YA AZAM MEDIA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofunga Maadhimisho ya Miaka 10 ya AZAM Media kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam, Desemba 17, 2023.
************

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewapongeza viongozi na  wafanyakazi wa kampuni ya Azam Media Limited kwa mafanikio lukuki waliyopata katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.

 

Amesema kupitia urushaji wa matangazo yake, kampuni hiyo imeweza kuwa mzalishaji mkubwa wa ajira kwa mawakala, wanataaluma mbalimbali, imeinua wanamichezo katika soka, masumbwi, mbio za magari na pikipiki, waigizaji wa filamu na wasanii wa muziki.

 

“Pia mmedhamini baadhi ya vilabu nchini, kuweka taa kwenye baadhi viwanja vya michezo hali ambayo imewezesha mechi za soka kuchezwa usiku. Msione hili kuwa ni jambo dogo,  AZAM mko mbali sana. AZAM mko juu,” alisema.

 

Alitoa pongezi hizo jana usiku (Jumapili, Desemba 17, 2023) wakati akifunga maadhimisho ya miaka 10 ya Kampuni ya Azam Media Limited yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

 

“Ninawapongeza Azam Media Limited kwa kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ajira kwa Watanzania kuanzia mawakala hadi watangazaji. Tunakutambua Azam Media Limited kama mdau mkubwa wa kutoa ajira,” alisema.

 

“Ninawapongeza pia kwa kubeba dhima ya kutunza mazingira kupitia kampeni yenu ya ‘Mito ni Maisha Yetu.’ Ninawapongeza kwa kuona maeneo nyeti na kuyaingiza kwenye mpango wenu wa mwaka yakiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya Azam Media Limited,” alisema.

 

Alisema kupitia kampeni hiyo, walihamasisha makundi ya jamii ili yashiriki kwenye uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji. “Lengo lilikuwa ni kujenga uelewa ili jamii ifanye shughuli zao za kibinadamu kwa kuzingatia umuhimu wa kutunza mito ambayo ni tegemeo kubwa kwa viwanda, kilimo, uzalishaji wa umeme na matumizi ya nyumbani. Naungana nanyi katika hili kwani haya ndiyo mambo ambayo Watanzania wanatakiwa kuyasikia na kuyazingatia wakati wote.”

 

Mapema, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye aliwapongeza wafayakazi wa kampuni hiyo kwa kuzingatia weledi katika utendaji kazi wao.

 

“Azam Media ni miongoni mwa vyombo ambavyo vinanipa usingizi mzuri kutokana na umahiri wao wa kazi, lakini pia niwapongeze kwa uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na kampuni hii ili kuhakikisha matangazo yao yanafika maeneo mengi.”

 

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa AZAM Media Limited (AML), Tido Mhando alisema maadhimisho hayo yalianza Januari mosi 2023 na waliyapanga yafanyike kwa mwaka mzima ili waweze kuufahamisha umma nini kimefanyika ndani ya miaka hiyo 10.

 

Alisema katika kipindi hicho, wameweza kujijenga kwa kiwango kikubwa na kwamba hivi sasa wanasikika kote Afrika Mashariki na Kati.

 

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa makampuni yanayounda Bakhresa Group, Abubakar Bakhresa aliwashukuru Watanzania wote kwa jinsi walivyoipokea kampuni ya AZAM na bidhaa zake.

 

“Tunaishukuru Serikali kwa kuweka milango yake wazi wakati wote. Pia tunawashukuru wadau wetu tunaofanya nao kazi kama Bodi ya Filamu, BASATA na wengineo,” alisema.

 

Alisema miaka 10 ya mwanzo ilikuwa ya kujifunza, ninaamini miaka 10 ijayo, itakuwa ya kuboresha na kuongeza mchango zaidi kukuza michezo na sekta nyingine.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofunga Maadhimisho ya Miaka 10 ya AZAM Media kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam, Desemba 17, 2023.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akizungumza katika Maadhimisho ya Maka 10 ya Azam Media kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam, Desembha 17, 2023.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea Tuzo Maalum ya Azam Media   kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Azam Media, Abubakar Bakhresa wakati alipofunga Maadhimisho ya Miaka 10 ya Azam Media kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam Desemba 17, 2023.  Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  akipata maelezo kuhusu picha zinazoonyesha historia ya Azam Media kutoka kwa Afisa  Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando, (kulia) kabla ya kufunga Maadhimisho ya Miska 10 ya Azam Media yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam, Desemba 17, 2023. 


Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Azam Media, Abubakar Bakhresa wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salam kufungua Maadhimisho ya miaka 10 ya Azam Media, Desemba 17, 2023. wa pili kushoto ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye na kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando. 

No comments:

Post a Comment