December 19, 2023

MKOA WA DODOMA WAKABIDHIWA GARI 5 KUHUDUMIA AFYA

 








Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa (MB) leo Desemba 19, 2023, amekabidhi gari 5 kwa Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kutumika kwenye shughuli za usimamizi wa huduma za afya. Hafla hiyo imefanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma.

Waziri Mhe. Mchengerwa amewataka waganga wa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma kuzitumia gari hizo kwa uadilifu kama ilivyokusudiwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi.

"Mhe. Rais amezitoa gari hizi 5 kwa Watanzania. Mpango wa Serikali ni kila Halmashauri kupokea gari moja na kila Jimbo la uchaguzi lipate gari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) 1. Mpaka Sasa Dodoma ilipokea gari 3 kwenye Halmashauri za Mpwapwa, Chamwino na Hospitali ya afya ya akili Mirembe, hivyo leo Halmashauri nyingine nazo zitapata gari hizi.

"Gari hizi zitumike kwa namna zilivyokusudiwa kwani ni maono ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ndio maana ametoa fedha nyingi kwa TAMISEMI kununua gari hizi. Takribani shilingi Bilioni 52 zimetolewa kununua gari 528 kati ya hizo 316 ni gari za kubebea wagonjwa na nyingine 212 kwa ajili ya kutumika na waganga wa Mikoa na Wilaya" amefafanua Mhe. Mchengerwa

Kadhalika, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amemshukuru Mhe. Rais kwa kutoa gari hizo kwa Mkoa wake kwani zitasaidia kurahisisha utoaji wa huduma za afya.

"Gari hizi zitawezesha usimamizi wa shughuli za miradi ya afya sambamba na kutoa huduma tembezi ndani ya Mkoa kwani Serikali imekua ikitoka fedha nyingi kwenye sekta ya afya hivyo tunaahidi kutunza gari hizi na kuzitumia kama ilivyokusudiwa.Mkoa wa Dodoma una hitaji gari 79 za kubebea wagonjwa ambapo mpaka Sasa tumeshapata gari hizo kwa asilimia 34. 

"Dhamira ya Mhe. Rais ni kutokomeza kabisa vifo vya watoto wachanga na Mama wajawazito wakati wa kujifungua ndio maana mkakati wa M- MMAM unasaidia usafirishaji wa watoto wachanga ulizinduliwa tarehe 26 April 2022 na umekua na mafanikio makubwa. Mkakati huu mpaka Sasa umeshanufaisha takribani wateja 1730" Amesema Mhe.Senyamule

No comments:

Post a Comment