Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na wafanya biashara wa Soko la Majengo kuhusiana na kufanya maboresho kulingana na hadhi ya Makao Makuu ya nchi kwani ni la miaka mingi sasa na tayari fedha zimeshatengwa kutoka Serikali kuu kwa ajili ya shughuli hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri akizungumzna na kusema soko hilo lina wafanyabiashara wapatao 220 ambapo kila mmoja anahudumia wateja kuanzia wanne hadi watano kwa siku.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema kuwa Soko la Majengo linatarajiwa kufanyiwa maboresho kulingana na hadhi ya Makao Makuu ya nchi kwani ni la miaka mingi sasa na tayari fedha zimeshatengwa kutoka Serikali kuu kwa ajili ya shughuli hiyo.
Hayo ameyasema Novemba 20, 2023 wakati wa ziara yake ya kutembelea Soko la Majengo lililopo Jijini Dodoma pamoja na kusikiliza kero za wafanyabiashara hao ikiwa ni utaratibu wake kutembelea makundi mbalimbali, kusikiliza na kutatua kero.
“Soko linakuja kujengwa kwa viwango vya majengo ya Dodoma Jiji kwa hadhi ya Makao makuu ya kisasa. Lazima huduma za soko hili ziendane na sura ya Makao Makuu ya nchi. Maboresho ni lazima yafanyike kwa utaratibu uliowekwa na Serikali wa kukaa, kushauriana na kukubaliana kwani yamo kwenye Sera ya nchi ya maboresho ya masoko”. Mhe. Senyamule
Katika ziara hiyo pia aliongozana na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri ambaye amesema soko hili lina wafanyabiashara wapatao 220 ambapo kila mmoja anahudumia wateja kuanzia wanne hadi watano kwa siku.
Soko hili linahudumia jumla ya wateja wanaoweza kufikia 10,000 kwa siku hivyo maboresho ni muhimu kufanyika kwenye soko hili ili mazingira yaweze kuwa rafiki kwa wateja.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Jiji Bw. Francis N. Kaunda katika taarifa yake amesema vyanzo vya mapato ya soko hili vinakusanywa moja kwa moja na Halmashauri ya Dodoma kutoka kwa wafanyabiashara na vingine vinakusanywa na wazabuni. Vyanzo hivyo ni pamoja na kodi ya pango kwa ajili ya vibanda na meza, ushuru wa vyoo, mizigo inayoingia sokoni pamoja na ada za mikataba.
Makisio ya mapato kwa mwaka ni Shilingi 204,700,629.00 na mpaka kufikia tarehe 10 Novemba 2023, zimepatikana Shilingi 156,151,500.00 ambazo ni sawa na asilimia 76 ya mapato ya mwaka pamoja na vyanzo tajwa hapo juu. Halmashauri ya Jiji la Dodoma hukusanya ada ya Leseni pamoja na ushuru wa huduma (service levy) kutoka kwa wafanyabiashara waliopo ndani ya soko wenye sifa za kupewa leseni.
Soko la majengo ni moja kati ya Soko kuu lililopo Mtaa wa Mausi, Kata ya Majengo ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Soko hili lilianzishwa mnamo mwaka 1996 kwa wafanyabiashara waliokuwa kwenye Soko la zamani eneo la Nyerere Square kuhamishiwa Soko la Majengo lenye jumla ya vibanda na meza zipatazo 1,328 na lina jumla ya wafanyabiashara zaidi ya 2,000. Soko hili ni ‘Soko Mama’ kwa masoko madogo madogo kuchukua bidhaa zao hapa.
No comments:
Post a Comment