Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema serikali itahakikisha inawalinda vijana kwenye soko la ajira kwa kuhakikisha ajira zao za kwanza kwenye utumishi zinazingatia vigezo vya utaalamu wa kada husika na sio uzoefu kazini.
Kikwete amesema hayo leo Jumatano Novemba 01, 2023 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Ngwasi Kamani aliyehoji kigezo cha kutakiwa uzoefu katika kuomba kazi kwa vijana waliohitimu vyuo kuwa ni ubaguzi kwa vijana wanaoanza kuomba ajira.
Huku akiwakumbusha Watanzania hasa Vijana wanaopambana katika soko la ajira kuwa zinatekelezwa kwa kuzingatia sera ya menejimenti na ajira ya mwaka 2008.
Kwa mujibu wa aya ya 4 kifungu cha 2 (i) inaelekeza kwamba ajira ya kwanza hususani kwa wale wanaoajiriwa kwa cheo cha kuanzia kwenye miundo ya serikali itafanyika kwa kuzingatia vigezo vya utaalamu bila kujali uzoefu isipokuwa kama ajira husika itahitaji kuwa na uzoefu.
Pamoja na hayo, Naibu Waziri huyo aliwakumbusha kuwa mara nyingi vigezo vinakuwa kwenye baadhi ya kada ya ubobezi kama Udereva na sio madaraja ya kuingia kazini.
No comments:
Post a Comment