Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Mhe. Remidius Mwema ikishirikiana na wadau mbalimbali, imeandaa Mashindano ya mbio za Marathon zitakazojulikana kama Kongwa African Liberation Marathon zitakazofanyika tarehe 25, Novemba 2023 huku mgeni rasmi akiwa ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbalo lengo likiwa ni kutangaza fursa mbalimbali za kiutalii zinazopatikana Wilayani humo.
Hayo yamebainishwa wakati wa Mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma hii leo Novemba 16, 2023 ambapo Mhe. Mwema amesema wameamua kuanzisha mashindano hayo kwani Kongwa ina historia kubwa kipindi cha harakati za kupigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika kama vile Msumbiji, Malawi, Afrika kusini, n.k
"Kongwa ni kielelezo cha kupigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika kwani kuna kambi ya kwanza ya wapigania Uhuru wakiwemo Sam Nujoma, Samora Machell, Nelson Mandela na wengine wengi. Pia fursa nyingine itakayotangazwa na mbio hizo ni uwekezaji kwani Kongwa inahitaji kujengwa kumbi kubwa za mikutano, hotel kwa ajili ya makazi kwani tunatarajia kumpokea wageni wengi mbalimbali baada ya Marathon hii."
Pia amefafanua fursa mbalimbali zinazopatikana katika Wilaya yake.
"Tuna mpango wa kuifanya Kongwa kuwa sehemu ya utalii kutokana na uwepo wa Handaki lililotumiwa na wapigania Uhuru, Kongwa ni lango la wageni wanaoingia makao makuu ya nchi, tuna soko la Kimataifa la mazao ya nafaka, Ranchi ya NARCO, viwanda zaidi ya 200 vya uchakataji mafuta na vielelezo vingine vingi vinavyoifanya Kongwa kuwa ya kiutalii na kuvutia wawekezaji zaidi" Ameongeza Mhe. Mwema.
Ametoa mchanganuo wa mbio hizo kwamba kutakua na mbio za umbali wa Km 5 kwa ajili ya watu wa rika zote, mbio za Km 10 na Km 21. Washindi nao wamegawanyika katika vipengele vya; kwa wanaume Km 21, mshindi wa kwanza atapata Shilingi Milioni 1, wa pili 600,000 na wa tatu 400,000 huku kwa upande wa Wanawake, mshindi wa kwanza atapata Shilingi 500,000, wa pili 300,000 na wa tatu 200,000
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Marathon Wilaya Kongwa Bw. Calvin John amesema maandalizi yamekamilika kwa asilimia 98 na watu wote wanakaribishwa kushiriki kwenye mbio hizo kwa kufanya usajili na kulipia shilingi 35,000 kupitia lipa namba 12296932 kwa njia ya mitandao yote ya simu au kwa Benki ya NMB. Aidha, fedha zitakazopatikana kupitia mashindano hayo zitatumika kukarabati majengo ya kihistoria, kuchangia mfuko wa Elimu wa Wilaya ya Kongwa na mengine mengi ya uboreshaji wa sekta ya Utalii.
No comments:
Post a Comment